Hospitali hizo zilitangaza jana kurejeshwa utaratibu huo kwa kile zilichodai kuwa hawakufikia makubaliano na serikali kupitia NHIF kuhusu mabadiliko ya vifurushi vipya vya mfuko huo vilivyotangazwa kuanza kutumika juzi.
Baadhi ya hospitali hizo zilizotangaza uamuzi huo kupitia Chama cha Watoa Huduma Binafsi za Afya Tanzania (APHFTA) ni Aga Khan, Masana, Regency Medical Centre, TMJ, Kairuki na Boch.
Baada ya kutangaza uamuzi huo, serikali kupitia Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, imesema bado kuna nafasi ya mazungumzo kuhusu jambo hilo na kuwataka wadau hao warudi kweye meza ya mazungumzo.
Kutokana na kauli hiyo, hospitali hizo zilitangaza kwamba zimerejesha utaratibu wa kuwapokea wanachama wa NHIF baada ya kuwapo mwanga wa kurejewa mazungumzo ili kufikiwa kwa mwafaka katika jambo ambalo lilisababisha kutokea kwa hali hiyo.
Hospitali ya Bochi katika tangazo lake, imesema imeendelea kutoa huduma kwa wagonjwa wote, walioko wodini na chumba cha uangalizi maalumu (ICU) na kwamba huduma za NHIF zimerejea kama kawaida.
Baada ya tangazo hilo, Waziri Ummy katika ukurasa wake wa X (zamani Twitter), aliandika: “Asanteni sana Bochi na wote mliorudisha huduma kwa wanachama wa NHIF. Tunawashukuru sana sana. Ninawaahidi kuwa tutafanya maboresho katika maeneo mahususi mtakayoainisha ndani ya muda mfupi.”
Aidha, uongozi wa Hospitali ya Kairuki, ulitangaza kuwa imerejesha huduma kwa wanachama wa NHIF baada ya kutangaza kusitisha kuanzia saa 6:01 juzi, muda rasmi uliotangazwa kuanza kutumika kwa vifurushi vipya vya mfuko huo.
“Taarifa hii (ya kurejeshwa kwa huduma) inakuja kufuatia (kutokana) na mazungumzo yanayoendelea kati ya serikali na APHFTA,” ilibainisha taarifa hiyo huku ikiwaomba radhi wagonjwa waliokosa huduma hiyo juzi.
Awali, NHIF katika taarifa iliyotolewa na Kaimu Meneja Uhusiano, Grace Michael, imesema vituo vilivyokuwa vimesitisha huduma hizo, vimerejesha huduma kama kawaida.
“Vituo hivyo ni Regency Medical Centre, Hospitali ya TJM, Hospitali ya Apollo na Bochi,’ imesema taarifa hiyo huku ikivikumbusha vituo vingine vilivyositisha, ambavyo vina mkataba wa kutoa huduma kwa wanachama wa NHIF, kurejesha mara moja.
HALI ILIVYOKUWA
Kutokana na tangazo la hospitali hizo kusitisha huduma kwa wanufaika wa NHIF, Nipashe ilishuhudia katika baadhi ya vituo hivyo wagonjwa wakizuiwa huku waliokuwa na uwezo wakitumia fedha taslimu ili kuepuka usumbufu pamoja na hali za ndugu zao.
Mwananchi mmoja, aliyejitambulisha kwa jina Collins Lema, aliyekuwa amempeleka mama yake mzazi katika hospitali moja (zilizotangaza kusitisha huduma za NHIF), alisema amelazimika kulipa Sh. 250,000 ili kuwezesha mzazi wake, mwenye tatizo la figo, kusafishwa damu.
Uchunguzi wa Nipashe pia ulibaini kuwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ilikuwa na wagonjwa wengi waliokuwa wakienda hapo baada ya kushindwa kupata huduma kwenye hospitali binafsi zilizotangaza kusitisha huduma.
Pia ilibainika kuwa wagonjwa wengi waliokwenda hapo, wengi walikuwa wenye maradhi sugu kama vile figo, hali ambayo ilisababisha wafanyakazi kufanya kazi za ziada huku kukiwa na foleni kwenye maeneo ya huduma hizo.
KAULI YA WAZIRI
Waziri Ummy baada ya kuwapo hali hiyo, aliwaagiza watoa huduma hao kuendelea kutoa huduma na endapo kuna shida katika kitita hicho, warudi katika meza ya majadiliano na serikali badala ya kusitisha huduma.
Ummy alisema gharama za mwisho ambazo zimewekwa katika kitita Januari 4, mwaka huu, alikutana na timu yake ya wataalamu wa wizara ambao walifanya kikao cha pamoja na wadau wa NHIF.
Alisema katika kikao hicho walikuwepo wamiliki wa vituo vya afya binafsi, Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC), Kamati ya Afya chini ya Bakwata, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Chama Cha Madaktari Tanzania (MAT) na NHIF kwa lengo la kusikiliza hoja za wadau.
Januari 4, mwaka huu, alisema wizara iliamua kusitisha utekelezaji wa kitita kipya cha NHIF cha mwaka 2023 na kuunda kamati yenye wadau kutoka serikalini, sekta binafsi na taasisi za bima kwa ajili ya kuishauri serikali.
“Kwa sababu hakuna vigezo vingine waje mezani watueleze tumewawekea faida ndogo kwa kutueleza dawa wamenunua kwa kiasi gani? na gharama za uendeshaji zipoje? waje waseme kama dawa hii haiuzwi bei fulani sio mseme hatutaki kitita. Leteni hoja zenu mezani. Kamati naipongeza imefanya kazi nzuri,” alisema Waziri.
“Nawaomba warudi kwenye meza ya mazungumzo. Kamati imeweka vigezo, waje waseme vigezo hivi havipaswi kutumika katika kutoa huduma za afya,” alisisitiza.
Ummy alisema baada ya kupata taarifa ya kamati aliitisha kikao kingine Februari 17 na kuwapatia taarifa hiyo, hakuna hata mmoja aliyesema hawakubaliani na vigezo hivyo.
Waziri Ummy alisema serikali imeielekeza NHIF kuendelea kupokea maoni ya wadau kuhusiana na kitita hicho wakati wa utekelezaji.
Naomba nieleze kumekuwa na ushirikishwaji mkubwa wa wadau katika mchakato huo nimewasikiliza mimi na timu yangu tangu mwaka 2022 tunachelewa lakini tumekuwa wavumilivu milango ya wizara ipo wazi,” alisema.