Ng’ombe wa mil. 20/- wakatwa mapanga, mchungaji ajeruhiwa

03Sep 2023
Ashton Balaigwa
MVOMERO
Nipashe Jumapili
Ng’ombe wa mil. 20/- wakatwa mapanga, mchungaji ajeruhiwa

NG’OMBE 13 wenye thamani ya Sh. milioni 20, mali ya wafugaji wa jamii ya Kimasai katika Kijiji cha Maharaka, Mvomero mkoani Morogoro, wamekatwakatwa na mapanga na mmoja wa wafugaji kujeruhiwa na kikundi cha watu ambao mpaka sasa hawajajulikana.

Baadhi ya wafugaji jamii ya Kimasaai wa kijiji cha Maharaka, kata ya Boma, wilayani Mvomero mkoani Morogoro, wakiangalia ng’ombe za wafugaji wenzao, zilizolala chini na kushindwa kutembea baada ya kukatwa na mapanga na kundi la watu wasiojulikana wakati wakizinyweshea maji katika Mto Maharaka jana. PICHA: ASHTON BALAIGWA

Mmoja wa wamiliki wa ng’ombe hizo, Mbayani Kipereni, mkazi wa Doma, alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa 6:30 mchana pembezoni mwa Mto Maharaka walipokwenda kunywesha maji ng’ombe hao na gafla wakavamiwa na kundi la watu.

Alisema baada ya kuvamiwa, kundi hilo lilianza kuwashambulia na kuwajeruhi wakiwa na mapanga na silaha mbalimbali huku wengine wakiwakatakata kwa mapanga ng’ombe hao na wakikimbia na mpaka sasa hawajulikani waliko.

'Tulikuwa tunapeleka ng’ombe katika eneo la kunyweshea ambako ni Mto Maharaka na hakuna eneo lolote la shamba lenye mto. Ghafla tulivamiwa na kundi kubwa la watu wakaanza kutupiga na wengine kukata ng’ombe mapanga,” alisema Kipereni.

Mmliki mwingine wa ng’ombe hao, Adam Nduli, alisema wanashangaa kuvamiwa na kundi hilo wakati eneo hilo la mto kwa miaka mingi wamekuwa wakitumia kunyweshea  mifugo yao.

Alisema wanashangazwa na kitendo kilochofanywa na kundi hilo kwa kuwa hakuna shamba lolote ambalo mpaka sasa limeharibiwa na mifugo, hivyo kuiomba Serikali kuingilia kati ili kuepusha kutokea kwa athari zingine.

Naye mmoja wa wafugaji kutoka Kata ya Doma, Kisonga Kipareni, alisema tatizo hilo limekuwa likichangiwa na baadhi ya viongozi wa kata ambao hakuwataja vyeo wala majina, kwa kuwazuia wafugaji kunywesha mifugo yao katika mto Maharaka wakati hakuna sehemu nyingine yenye maji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi (ACP) Alex Mkama, alikiri kuwepo kwa tukio hilo alilosema limefanywa na kundi la wahalifu ambao mpaka sasa hawajulikani.

Mkama alisema kundi hilo liliwavamia wafugaji hao na kukatakata ng’ombe kwa mapanga na kumjeruhi mmoja wa wafugaji kati ya wawili waliokuwa wakinywesha mifugo yao.

Alisema mpaka jana mchana, ng’ombe 13 walikuwa wamekatwakatwa mapanga na tayari jeshi hilo limeanza msako dhidi ya waliofanya tukio hilo na kuendelea kuimarisha ulinzi katika eneo hilo.