Akizungumza na Nipashe jana, Ofisa Uhusiano wa MOI, Patrick Mvungi alibainisha kutokujitokeza kwa ndugu wa mgonjwa huyo ambaye afya yake inaendelea kuimarika.
"Majeruhi huyu bado yupo ICU na afya yake inaendelea kuimarika lakini ndugu zake mpaka sasa hawajajitokeza," alisema.
Ajali hiyo ilitokea Jumatano ya wiki hii eneo la Kisutu, ikihusisha gari ndogo aina ya Rav 4 lenye namba ya usajili T 978 DHZ na basi la mwendokasi lenye namba za usajili T 122 DGW.
Video fupi iliyorekodi tukio hilo lililotokea majira ya saa 12:31 asubuhi, ilionyesha namna ajali hiyo ilivyotokea kwa magari hayo kugongana, basi la mwendokasi likipoteza mwelekeo na kwenda kumgonga mwenda kwa miguu huyo, mwanamume aliyekuwa akipita maeneo hayo kisha kwenda kugonga ukuta wa maduka.
Wakati wa ajali hiyo basi la mwendokasi lilikuwa linatokea Kivukoni kuelekea Kimara na dereva wa gari dogo aliingia barabara ya mwendokasi bila kuchukua tahadhari, hivyo kusababisha ajali hiyo iliyowaacha watu 37 wakijeruhiwa.










