Amesema ACT-Wazalendo kimefuata misingi na taratibu sahihi za demokrasia kwa kuandaa mfumo mzuri wa kuwapata viongozi ili kujaza nafasi zilizoachwa wazi ndani ya chama hicho.
Aliyasema hayo jana wakati wa Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho uliofanyika mkoani Dar es Salaam, uliokuwa na lengo la kufanya uchaguzi wa viongozi wa ngazi za juu.
Viongozi hao ni Mwenyekiti wa ACT –Wazalendo Taifa, ambaye atakuwa mrithi wa Hayati Maalim Seif Sharif Hamadi, nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar pamoja na mjumbe mmoja wa Halmashauri Kuu.
Akihutubia katika mkutano huo, Nyahoza, aliipongeza ACT-Wazalendo kwa kufuata misingi na taratibu sahihi ya demokrasia kwa kuandaa mfumo mzuri wa kuwapata viongozi hao.
Nyahoza alisema mfumo unaotumiwa na chama hicho ni wa ushindani, ustaarabu kwa watu kugombea katika nafasi mbalimbali.
“Tunawapongeza kwa kuandaa mkutano huu, nimehudhuria mikutano mingi ya vyama vya siasa huu umepangwa vizuri. Kuandaa mkutano mkuu siyo jambo dogo, pia tunawapongeza kwa kuheshimu na kutekeleza matakwa ya kidemokrasia kwa sababu tunaelewa tulipata tatizo kubwa kama nchi la kuondokewa na Hayati Maalim Seif Sharifu Hamad,” alisema Nyahoza.
Aidha, alitoa wito kwa vyama vingine vya siasa kuiga mfumo huo na kuweza kuboresha suala la demokrasia, akisema kwamba bado kuna changamoto ya demokrasia katika vyama vya siasa.
“ACT-Wazalendo ni kati ya vyama ambavyo vina ukomavu mkubwa wa kisiasa, mnafanya siasa ya kistaarabu, mmetoka kwenye uchaguzi pamoja na changamoto za wakati ule lakini mkaingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa, tuliandaa mkutano wa wadau pale Dodoma mlishiriki ule ni ukomavu wa kisiasa,” alisema Nyahoza.
Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliwashukuru wanachama wa chama hicho wa ndani na nje ya nchi kwa michango yao iliyowezesha suala hilo kukamilika, akidai kuwa bila ushirikiano wao mkutano huo usingefanikiwa.
Alisema licha ya madhila waliyokutana nayo nyakati za nyuma lakini waliamua kusimama imara na kuwa na umoja ambao umewawezesha kufika walipo sasa.
Zitto alisema: “Wakati tunajenga chama ni lazima tuendeleze agenda za kitaifa, kwetu sisi tunajenga chama wakati tunapambania mabadiliko ya kisheria na kisiasa, tunatambua umuhimu wa katiba mpya.
“Tuhakikishe uchaguzi unaofuata uwe na tume huru ya uchaguzi, sisi ni lazima tuwe na kila aina ya mbinu, tutaheshimu sheria za haki lakini hatutaheshimu sheria ambazo zinaminya haki za watu.” alisema










