Taarifa hiyo imetolewa leo Januari 08, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme, wakati wa ziara yake ya kukagua mahudhurio ya wanafunzi ambao wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu pamoja na uandikishaji wa wanafunzi wa awali na darasa la kwanza katika shule mbalimbali ikiwamo na shule ya Sekondari ya wasichana.
Mndeme akiwa katika shule hiyo ya Sekondari ya Wasichana iliyopo Butengwa Manispaa ya Shinyanga, amesema amesikitishwa na kitendo cha mzazi mmoja (jina lake limehifadhiwa) kutaka kukatisha ndoto za mtoto wake kwa tamaa ya kupata mahari ya ng’ombe 15 na kuamua kumuozesha.
“Mwanafunzi huyu jina lake tumelihifadhi amepata ufaulu daraja “A” lakini cha kusikitisha baba yake mzazi hataki asome na kuamua kutaka kumuozesha kwa mahari ya ng’ombe 15, lakini ndoa hiyo haikufanikiwa ili tibuliwa na mwanafunzi kwa sasa yupo shuleni akiendelea na masomo yake ya kidato cha kwanza,” amesema Mndeme.
Ameongeza kuwa baba mzazi wa mwanafunzi huyo wanamtafuta sababu alikimbia kusikojulikana baada ya kusikia akitafutwa na vyombo vya dola na kubainisha kwamba Serikali inaendelea kumsaka na akipatikana atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Aidha, Mndeme ametoa wito kwa wazazi na walezi mkoani humo kuacha tabia ya kuozesha wanafunzi ndoa za utotoni bali wawaache wasome ili watimize ndoto zao, na hata kuja kuwa viongozi wa baadae wa taifa hili.
Nao baadhi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza ambao wanasoma shule ya Sekondari ya Wasichana Shinyanga, wametoa wito kwa wazazi wasiwabague watoto wa kike katika suala zima la kupata elimu, bali watoto wote wa kiume na kike wanahaki sawa ya kupata elimu na kuziishi ndoto zao.
Naye Mkuu wa shule ya Sekondari ya Wasichana Shinyanga, Nurah Kamutu, amesema shule hiyo imepangiwa wanafunzi wa kidato cha kwanza 143, lakini mpaka sasa wamesharipoti wanafunzi 10.










