Akizungumza na Nipashe mapema wiki hii, Prof. Mchome alisema Wizara haiwezi kufanya chochote kwa sasa hadi watakapokabidhiwa mapendekezo kutoka kwenye bodi hiyo.
“Tunasubiri ushauri wa bodi kama wataamua serikali ikate rufaa au la, lakini kama mkataba wake wa kazi labda uliisha, wao ndo watatueleza tufanye nini,” alisema.
Saliboko aliachiwa huru baada ya kushinda kesi ya tuhuma za kupokea rushwa ya Sh. milioni 40.4 kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira.
Saliboko aliachiwa mapema mwaka huu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kumuona hana hatia.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, aliyesema mahakama imemuona mshtakiwa hana hatia kutokana na upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha shtaka dhidi yake pasi na kuacha shaka yoyote.
Hati ya mashtaka ilidai Februari 5, mwaka 2014 katika Benki ya Mkombozi, iliyoko wilayani Ilala, Dar es Salaam, akiwa Mtendaji Mkuu wa RITA alipokea Sh milioni 40.4 kupitia akaunti ya VIP Engineering ya Rugemalira.
Ilidaiwa alipokea fedha hizo kutokana na kazi yake kama bosi wa RITA wakati IPTL ilikuwa mfilisi na yeye alishughulikia hilo.
Tangu ashinde kesi hiyo, RITA bado imeendelea kuongozwa na Kaimu Mtendaji Mkuu, Emmy Hudson.










