Mtaalamu afichua midoli ina sumu

16Oct 2022
Mary Geofrey
Bukoba
Nipashe Jumapili
Mtaalamu afichua midoli ina sumu
  • Ni chanzo figo kuharibika, fizi kuwa za buluu

OKTOBA 23 hadi 27 kila mwaka, dunia huadhimisha wiki ya kuzuia sumu ya madini ya risasi. Nchini madhara makubwa yametajwa kuwapata watoto kupitia midoli ya kuchezea na rangi za ukutani.

Mratibu wa Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Yohana Goshashy, katika mazungumzo mahsusi na Nipashe mjini hapa jana, alieleza kwa kina ukubwa wa tatizo hilo nchini.

Anasema watoto wanapata sumu hiyo kwa kucheza katika maeneo yenye rangi inayobanduka kwa sababu wanaweza kuibandua kwa mikono na kuiweka mdomoni.

"Wakishika wanatakiwa kunawa kwa maji na sabuni kabla ya kula chakula ili kuepuka madhara," Goshashy anashauri na kubainisha kuwa midoli ya kuchezea watoto ina sumu ya madini ya risasi, hivyo bila kufahamu watoto hupata madhara.

Anasema kuwa ili kuepuka tatizo hilo, kunatakiwa kuwapo sheria na sera za kuzuia matumizi ya rangi au midoli ya watoto yenye madini ya risasi.

"Pawe na alama ya kuonyesha rangi zisizo na madini ya risasi katika vifungashio," Goshashy anasisitiza.

CHANZO CHA SUMU

Madini ya risasi hupatikana kwenye gamba la uso wa dunia; kwa watengenezaji wa betri za magari na redio; kwa wahunzi; watengenezaji wa glasi; rangi za kuta hususani zinazoondolewa.

Goshashy anasema vyanzo vingine vya sumu ya risasi ni pamoja na rangi ya kuchimba au rangi ya kale ya risasi katika nyumba ambazo zilijengwa kabla ya rangi ya risasi kupigwa marufuku mwaka wa 1978 kwa baadhi ya nchi.

Gushashy anataja chanzo kingine cha kawaida cha risasi ni maji ya kunywa, ikiwa yanatolewa kupitia mabomba ya zamani ya risasi.

"Kwa sababu risasi haiharibiki baada ya muda, udongo katika yadi au kando ya barabara unaweza kuwa na risasi, tangu siku ambazo petroli ilikuwa na madini ya risasi au kama matokeo ya vipande vya rangi ya risasi kutoka maeneo ya zamani ya viwanda na nyumba," anafafanua.

Anasema kuwa kutokana na madhara ya sumu ya madini ya risasi, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeziunganisha nchi kufanya madhimisho ya kuzuia sumu ya madini ya risasi duniani kwa kutenga wiki ya Oktoba 23 hadi 26 ya kila mwaka kujenga uelewa wa kuzuia matukio ya sumu ya madini ya risasi.

Goshashy anasema kaulimbiu kwa mwaka huu ni 'Sema hapana kwa matukio ya sumu ya madini ya risasi', akisisitiza kuwa Kituo cha Kitaifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu kinaunga mkono kaulimbiu hiyo kwa kutoa elimu ya kujikinga kupitia vyombo vya habari.

DALILI ZA SUMU

Goshasy anasema kwa kawaida sumu ya madini ya risasi hurundikana mwilini na hukaa kwa muda wa miezi au miaka kadhaa na haina faida yoyote kwenye mwili wa binadamu.

Anasema sumu hiyo inaweza kuathiri ubongo na viungo vingine muhimu na kusababisha mabadiliko ya mishipa ya fahamu (neva) na tabia, ugonjwa wa utumbo, kuharibika kwa figo na ucheleweshaji wa ukuaji hususani kwa watoto.

Alisema dalili za sumu hiyo mara nyingi huwa hafifu na ni ngumu kuzigundua kwa sababu zinafanana na za magonjwa mengine.

Goshashy anataja dalili hizo kuwa ni kuwashwa au hisia za ganzi (neuropathy), uchovu, kuumwa na kichwa, kupoteza umakini, upungufu katika kumbukumbu ya muda mfupi, kizunguzungu na kupoteza uratibu wa mwili.

Anataja dalili zingine kuwa ni kukosa uwezo wa utambuzi wa ladha mdomoni na fizi kupata mstari wa bluu, hali inayojulikana kama mstari wa Burton.

Anasema mwenye dalili hupata maumivu ya tumbo, kichefuchefu na kutapika, kuhara au kuvimbiwa na watoto wadogo hupata mabadiliko makubwa ikiwamo kushindwa kufanya vizuri darasani, tofauti na watoto wasio na tatizo hilo.

Goshashy anasema wakati mwingine mtu hupata ulemavu wa kudumu wa kiakili, kupata shinikizo la damu, kutosikia, mtoto wa jicho, utasa kwa wanaume, kuharibika kwa mimba na watoto kuzaliwa kabla ya wakati.

MBINU KUBAINI TATIZO

Goshashy anasema sumu ya risasi inaweza kutambuliwa kupitia aina mbalimbali za vipimo vya maabara za afya na kiuchunguzi ikiwamo Maabara ya Uchunguzi Sumu ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na  mashine za X-Ray.

Anasema vipimo hivyo ni vile vya mkusanyiko wa risasi kwenye damu ambavyo hutumia (μg) kwa kila desilita (dL) ya damu.

MATIBABU YAKE

Goshashy anasema njia kuu ya matibabu ya sumu itokanayo na madini ya risasi ni tiba inayoitwa kwa kitaalamu 'Chelation'.

Anasema tiba hiyo inahusisha matumizi ya mawakala wa 'chelating' ambayo hufunga kikamilifu chuma na kuunda kiwanja kisicho na sumu ambacho kinaweza kutolewa kwa njia ya mkojo kwa urahisi.

"Mfano wa wakala wa Chelation ni EDTA (asidi ya ethylene diamine tetra-asetiki)," anatoa ufafanuzi wa kitaalamu.

KUZUIA SUMU

Goshashy anasema wananchi wanatakiwa kuwa na utaratibu wa kujua afya zao na kuwa na taarifa kama walishawahi kuwa katika mazingira ya sumu hiyo.

Anasema kama watu wanaamini walipita katika maeneo hayo, wanatakiwa kutoa taarifa katika Kituo cha Kitaifa cha Kudhibiti matukio hayo.

Anasema jamii pia inatakiwa kuhakikisha familia inakula vyakula vya viwango vya juu vya madini ya Calcium, chuma na Vitamini C.

"Virutubisho hivi husaidia kupunguza viwango vya risasi katika damu na hivyo vinaweza kupunguza hatari ya sumu ya risasi," anafafanua.

Goshashy anasema jamii inatakiwa kuepuka kuwa na matumizi ya mabomba ya risasi katika maeneo inakoishi au kufanya kazi.

Pia anasema waliokutana na tatizo hilo, wanatakiwa kuzingatia matibabu ya haraka ili kuepuka kupata madhara zaidi.

Anatoa rai kwa jamii kubadili tabia ya kutokuchua tahadhari ya kuepuka sumu ya risasi.

USULI

Madini ya risasi yamekuwa na madhara kwa miaka mingi na jitihada za kuyapunguza zilianzishwa na mashirika mbalimbali ya kimataifa.

Mkataba wa kimataifa wa kudhibiti matumizi ya risasi nyeupe uliidhinishwa katika Kongamano Kuu la Shirika la Kimataifa la Kazi (ILO) tangu mwaka 1921 na kuridhiwa na mataifa 63.

Goshashy anawataka wananchi kutoa taarifa wanapokutana na matukio ya sumu za madini ya risasi kwa kupiga simu bure namba 022 2221410 na 0736 613333 ili kupata msaada wa haraka.