Mwanasheria Mkuu wa NECM, Heche Suguta, na wenzake watatu walisimamishwa kazi na Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira mwezi uliopita. Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya NEMC ambazo Nipashe inazo, Suguta alirudishwa kazini siku nne tu tangu kusimashwa kazi. Chanzo hicho ambacho hakikutana kutajwa jina gazetini kwa sababu si msemaji wa Baraza, Suguta alirudi kazini Januari 29. Ilikuwa ni siku nne baada ya Wizara hiyo kutangaza kumsimamisha kazi ili kupisha uchunguzi, baada ya kutuhumiwa kukiuka miiko ya kazi katika kusimamia kiwanda cha kusindika minofu ya punda kilichopo mkoani Dodoma. “Heche yuko kazini tangu Ijumaa ya wiki iliyopita, alikaa nyumbani siku nne tu ila hatufahamu nini kilitokea juu ya hilo,” kilibainisha chanzo hicho ambacho kilieleza kuwa hawana taarifa za maofisa wengine kama watarudishwa kazini au la. Gazeti hili lilifika katika ofisi za NEMC Mikocheni kutaka kujiridhisha kuhusu kurejea kwake kazini na kumkuta akiendelea na kazi zake kama kawaida, ingawa alikataa katakata kulizungumzia suala hilo. Alipoulizwa na Nipashe kuhusu ofisa huyo kurudishwa kazini, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Bonaventura Baya, alisema hawezi kuzungumzia jambo hilo kwa madai kuwa liko juu ya uwezo wake. “Siwezi kulizungumza suala hilo maana liko juu ya uwezo wangu, waulize mabosi wangu. Mimi sina cha kusema kwa sasa,” alisema Baya. Maofisa wa wizara hiyo hawakupatikana kuzungumzia suala hilo kwa siku mbili zilizopita. Wengine waliosimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi ni Ofisa Mazingira Mwandamizi Dk. Eladius Makene na Ofisa Mazingira, Boniface Benedict Kyaruzi. Katika adhabu hiyo pia Mkurugenzi Mkuu Baya aliagizwa kuandikiwa barua ya onyo kali la mwisho kwa tuhuma ya udhaifu wa usimamizi wa watumishi wa NEMC. Kuhusu kiwanda cha kusindika minofu ya punda mkoani Dodoma, taarifa hiyo ilisema imegundulika kuwapo kwa ukiukwaji mkubwa wa makusudi na wa wazi wa miiko ya kazi kwa watumishi wa NEMC Aidha, wizara iliagiza kuwa ndani ya wiki moja NEMC ipitie upya orodha ya wataalamu na taasisi elekezi, zilizosajiliwa na kufuta wataalamu na taasisi zote ambazo zimekuwa zikikiuka maadili ya kazi zao. Heche alijizolea umaarufu wakati wa zoezi la bomoa bomoa lililoanza Desemba mwaka jana ambapo mamia ya nyumba zilizojengwa sehemu za mabondeni zilivunjwa. Katika bomoa bomoa hiyo zaidi ya nyumba 600 zimeshabomolewa katika Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, huku Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Ardhi ikisitisha kuendelea kwa bomoabomoa ya nyumba zilizoko mabondeni. Kesi ya msingi ilifunguliwa na Mbunge wa jimbo hilo, Maulid Mtulia na wakazi wengine kupinga bomoabomoa kwa zaidi ya nyumba 15,000 zinazotarajiwa kubomolewa. Bomoabomoa hiyo iliyoanza Desemba 17 mwaka jana, ilianza na ubomoaji wa nyumba 300 katika bonde la Mkwajuni wilayani humo, na ilianza tena kwa kwa kasi baada ya kusitishwa kwa siku 14 kupisha wananchi kujiandaa kwa kubomoa zaidi ya nyumba 300, jumla kufikisha idadi ya nyumba 600. Ofisa Mazingira Mwandamizi Mkuu wa Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Arnold Kisiraga, alisema nyumba zaidi ya 15,000 zimekwishawekewa alama ya X, katika maeneo ya Buguruni kwa Mnyamani, Vingunguti na Tabata Segerea kisha maeneo ambayo wananchi wamejenga mabondeni Mto Msimbazi wote.
Msimamizi mkuu bomoabomoa arudishwa kazini
06Feb 2016
Nipashe
Msimamizi mkuu bomoabomoa arudishwa kazini
MSIMAMIZI Mkuu wa Operesheni ya bomoabomoa ya nyumba 600 zilizokuwa katika eneo hatarishi la bonde la Mkwajuni la Mto Msimbazi, jijini Dar es Salaam amerudishwa kazini siku nne tu tangu aliposimamishwa kazi na serikali kwa tuhuma za kukiuka maadili katika tukio tofauti.










