Mshona viatu akabidhiwa kiti mwendo

15Feb 2024
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Mshona viatu akabidhiwa kiti mwendo

SHIRIKA la Sauti ya Mama Afriika Foundation (SAMAFO) kwa kushirikiana na Elimisha, wamempatia kiti mwendo, Erineus Mhagama, mkazi wa Meta, jijini Mbeya, ili kumuondolea adha aliyokuwa anaipata kwenye shughuli zake za kila siku.

Erineus, ni mke na baba wa watoto wawili, alisema kwamba shughuli zake ni kushona na kufanyia marekebisho viatu, huku awali ikimpasa kutambaa chini muda mwingi akitekeleza majukumu yake.

“Sasa ninaweza kutoka hapa kwenda Mwanjelwa kutafuta mali ghafi kama soli. Awali hata mvua ikinyesha nilitambaa chini, magoti, nguo nililowa. Mbali na msaada huu pia ningeomba niongezewe mtaji, ili kulea familia yangu,” alisema Ernest.

Mkurugenzi Mtendajji wa SAMAFO, Tabitha Bugali, aliiambia Nipshe kwamba, wamempatia Erineus kiti hicho kwa kuwa ni mjasiriamali, ambaye anamahitaji hayo, ili kurahisisha majukumu ya kujitafutia kipato.

“Hiki ni kitenmdo cha upendo katika msimu huu, hasa mwezi wa wapendanao, tumeamua kumchagua Erineus,” alisema Bugali.

Mkurugenzi wa Elimisha, Debora Mwanyanje, alisema kwamba wameshirikiana na taasisi hiyo, kumpatia kiti hicho Erineus, baada ya kutuma maombi kutoka mashirika ya nje na miongoni mwa walivyowapatia ni kiti mwendo, ambacho amepewa Erineus.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Meta, Ester Mwaipungu, alisema kwamba kitendo cha kumpatia kiti hicho mkazi wa eneo lake, kimeonyesha upendo.

“Ipo TASAF kuwasaidia watu kama hawa wenye mahitaji, lakini bado haitoshi, uwapo wa taasisi kama hizi zinasaidia kuwatatulia watu matatizo yao kijamii,” alieleza Ester.