Akizungumza katika uzinduzi wa mradi wa Audity Accountability initiative (AAI) uliozinduliwa katika ngazi ya halmashauri ya wilaya ya Tanganyika Mkurugenzi wa UDESO Eden Ezekiel amesema mradi utaangazia utekelezaji wa mapendekezo yaliotolewa na mdhibiti na mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali kupitia ripoti ya ukaguzi ya 2017 juu ya uboreshaji wa miundombinu ya shule ili kuleta ufanisi katika sekta ya elimu.
Nae Afisa mradi Francis Mlumanga amesema mradi utakua na kazi saba za kufanya ikiwemo kuzijengea uwezo kamati zitakazo chaguliwa katika vijiji husika.
Tekla Mleleu ni Afisa Ufuatiliaji na Tathimini kutoka Taasisi ya WAJIBU amesema ripoti ya CAG ilibainisha shule mbili za msingi katika halmashauri ya wilaya ya Tanganyika ambazo ni Kasekese na Lugonesi hivyo mradi utaanza na shule hizo ili kutatua changamoto zilizopo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Alson Uisso amewataka madiwani, wenyeviti na watendaji kutoa ushirikiano kwa Taasisi hiyo ili mradi huo ulete matokeo chanya kwa serikali na jamii kwaujumla.
Mradi wa AAI utagharimu kiasi cha shilingi milioni 85 na elfu sabini na tano na utatekelezwa kwa kipindi cha miezi sita katika halmashauri ya wilaya ya Tanganyika hasa vijiji vya Kasekese na Lugonesi.









