Dk. Mkindi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi Kilele ya Kilimo cha Maua, Mboga, Matunda, Viungo na Mazao yatokanayo na Mizizi (TAHA), kila mwaka vyuo vyote vya kati na vile vya elimu ya juu hapa nchini, vinazalisha takribani wahitimu 700,000.
Hayo amezungumza jana na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), wakati alipokwenda kufunga tamasha la siku ya vipaji na ubunifu inayoandaliwa na chuo hicho kila mwaka.
“Umefika wakati vijana kufundishwa elimu itakayowasaidia kuwa wabunifu ili waweze kujiajiri. Hapa nchini, vyuo nilivyovitaja vinazalisha wahitimu hao, na kati hao 700,000, vyuo vya juu pekee yake kwa mwaka 2018, vilizalisha wahitimu 49,000, mwaka 2019 vilizalisha wahitimu 51, 000, mwaka 2020 vilizalisha wahitimu 48, 000; na kati ya hawa wote wanaoajiriwa ni chini ya asilimia 10 kila mwaka, "alisema na kuongeza kuwa;
“Kutokana na ongezeko hili la vijana wengi wanaohitimu vyuo vikuu, ukilinganisha na ajira, ipo haja kwa vijana, kuondoa dhana ya kuajiriwa na kuanza kufikiri kujiajiri.
Wajengwe uwezo waje na mawazo mbadala ya kujiajiri kupitia ubunifu, wanaoanzisha katika mazingira wanaoishi.”
Katika nasaha zake, Dk. Mkindi, ameishauri Menejimenti ya MoCU, kufikiria kutenga fedha kwa ajili ya Mradi wa Ujenzi wa Kituo Atamivu (Enqubation Hub), ambacho kitasaidia kukuza na kulea vipaji na ubunifu mwingine.
“Machi mwaka huu nilikuwa nchini Ufaransa, nilitembelea kituo kikubwa kuliko vyote cha kulea vipaji Barani Ulaya. Vipaji vinalelewa pale, na watu wanakwenda kuongeza uwezekano wa kupata ajira, kutokana na ongezeko la viwanda. Hata sisi tunaweza kufanya hivyo, na tutapata matokeo chanya kwa vijana wetu,”alishauri Dk. Mkindi
Awali, Mkurugenzi Huduma za Wanafunzi wa MoCU, Dk. Elisifa Nnko, alisema endapo vijana hao watapewa fursa katika maeneo mbalimbali, wanaweza kutengeneza ajira kwa wengine.
Pia, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho, Zahoro Shemahonge, akizungumzia tamasha hilo, aliwasihi waajiri kutoka sekta binafsi, kuungana na serikali kuhakikisha wanawasadia vijana kutokana na kazi wanazozifanya.










