Akiwa eneo la Nansio, Mjumbe wa Kamati Tendaji ya CHADEMA Kanda ya Ziwa Victoria, Karoli James, alimweleza Mbowe kwamba huduma za afya visiwani humo hairidhishi, hali inayosababisha baadhi ya wanawake kujifungulia ziwani wakienda maeneo mengine kuzifuata.
“Ukerewe tuna vijiji 75, kata 25 lakini tuna vituo vya afya vinne na zahanati 28. Bado tuna shida kubwa kwenye eneo la afya. Kuna jenereta la hospitali ya wilaya ambalo limenunuliwa kwa Sh. milioni 60 lakini bovu kwa muda mrefu hali inayosababisha watu wanapokuwa kwenye vyumba vya upasuaji kukosa huduma pale umeme unapokatika,” alisema.
James aliomba serikali iangalie namna ya kuzitatua changamoto hizo kwa kuwapelekea jenereta lingine na kuongeza vituo vya afya kulingana na idadi ya vijiji na watu waliopo huko ili kuokoa maisha ya wajawazito.
Akizungumza katika mkutano huo, Mbowe aliwataka wananchi kusamehe utawala uliopita kwa yote kwa kuwa ulishindwa kuyafanya kwa kile alichokiita kuwa ni tatizo la miongozo ya chama tawala.
Mbowe alisema endapo watakiamini, chama hicho kitahakikisha kinabadilisha mifumo mizima ya utawala ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa kusoma mapato na matumizi katika kila kipindi cha utekeleza ili kuweka uwazi wa kila mwananchi kuelewa na kuondoa hali ya ubadhirifu.
Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Bara, Tundu Lissu, aliendelea na mikutano yake katika mikoa ya Mwanza na Mara na kuwapa wananchi elimu kuhusu mkataba baina ya Tanzania na kampuni ya DP World.
Oparesheni ya +255 Katiba Mpya Okoa Bandari kwa awamu ya pili inayoendelea katika mikoa ya Kanda ya Ziwa inatarajia kuhitimishwa leo viwanja vya Furahisha.










