Mkaguzi wa Dawa wa TMDA Kanda ya Mashariki, Japhari Mtoro, alisema hayo jana wakati wa operesheni hiyo iliyohusisha pia Jeshi la Polisi huku akibainisha kuwa mtuhumiwa huyo alikutwa na dawa mbalimbali, nembo na vifungashio vyake.
Alisema mtuhumiwa anadaiwa kutengeneza na kusambaza dawa hizo mijini, vijijini na nchi jirani na kwamba alikamatwa baada ya uchunguzi uliofanywa na TMDA.
"TMDA ilikuwa inamtafuta Williams Mwangile mkazi wa Matembele Lodge eneo la Kipawa kwa kosa la kuzalisha dawa bandia kwa mfumo wa makopo kinyume cha kifungu 76 cha Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba Sura ya 219," alisema Mtoro.
Alisema baada ya kumkamata mtuhumiwa huyo, walimfanyia uchunguzi katika nyumba yake na nyumba ya wazazi wake.
“Nyumbani kwake tulikuta lebo (nembo) 537 ambazo zina majina ya dawa mbalimbali ambazo zimepigwa chapa lakini pia tulikuta makopo matupu 12 ambayo yanatumika kufungasha dawa," alisema Mtoro.
Alitaja vitu vingine kuwa ni viroba vitatu, kimoja cha unga wa njano na viwili unga mweupe.
Alisema nyumbani kwa wazazi wake, walikuta vifungashio vitupu ya dawa aina ya rangi mbili.
“Nyumbani kwa wazazi wake tumekuta lebo 142, hivyo kufikisha jumla ya lebo 679. Baada ya kumpata mtuhumiwa ataunganishwa na wenzake na kufikishwa mahakamani," alisema Mtoro.
Mkaguzi huyo aliwashukuru wadau na viongozi wa serikali ya mtaa, Jeshi la Polisi, wananchi kwa ushirikiano mkubwa walioutoa hadi kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo ambaye walikuwa wakimtafuta tangu mwezi uliopita
Mjumbe wa Shina Na. 6 wa Mtaa wa Matembele ya Kwanza, Marygrory Mambo, ambaye ndiye aliyeshirikiana na TMDA na Jeshi la Polisi kwenye upekuzi huo, aliomba wananchi waendelee kutoa taarifa kwa mamlaka hiyo, kufichua wahalifu wa aina hiyo.










