Matatani  kutaka kumuua mtoto baada ya  kujifungua ili kunusuru ndoa

19Jan 2024
Neema Hussein
NSIMBO
Nipashe
Matatani  kutaka kumuua mtoto baada ya  kujifungua ili kunusuru ndoa

Msichana  mwenye umri wa miaka 19 aliyetambulika kwa jina la Rehema Erick mkazi wa Mtapenda Halmashauri ya Nsimbo mkoani Katavi ameingia matatani kwa kujaribu kumuua mtoto wake kwa kumtupa  chooni baada ya kujifungua ili kulinda ndoa yake isivunjike.

Akizungumzia tukio hilo mama wa binti huyo Winfrida Amosi  amesema alipigiwa simu na mume wa binti yake kuwa mwanae anaumwa tumbo hivyo wameenda  hospitali  ya wilaya kwaajili ya matibabu pasipo kujua kuwa aliolewa akiwa na mimba ya mwanaume mwingine akiwa huko ndipo alipatwa na uchungu kisha kwenda chooni kujifungua na kufanya ukatili huo.

Ester Julius ni shuhuda wa kwanza katika tukio hilo amesema alikua akifanya usafi ndipo aliona damu chooni baadae akaona mtoto ambae alikua amefichwa nyuma ya sinki la kunawia nakutoa taarifa kwa wahudumu wa afya katika hospitali hiyo.

Kaimu Mganga Mkuu Hospital ya Wilaya Nsimbo Grory Sollo  amesema mtoto huyo anaendelea na matibabu kutokana na majeraha aliopata ikiwa ni pamoja na kuvunjika miguu huku  Afisa Ustawi Halmashauri ya Nsimbo Theresia Mwendapole akidai ni tukio la kwanza kutokea ndani ya mwaka huu.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusuph ameagiza kukamatwa kwa binti huyo kutokana na kufanya jaribio la kutaka kuua.