Mambo 13 alama Edward Lowassa kukumbukwa

17Feb 2024
Godfrey Mushi
Dodoma
Nipashe
Mambo 13 alama Edward Lowassa kukumbukwa

LINAPOTAJWA jina la Edward Ngoyai Lowassa, ni dhahiri pasipo na shaka kuna baadhi ya taswira ya mambo yanakuja ambayo kiongozi huyo aliyafanya na yatakuwa alama ya kudumu kwa kizazi cha sasa na vinavyofuata. Kwa maneno mengine, matendo yake yatabaki kuwa historia na alama ya kumbukumbu isiyofutika.

Mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Azizi akitoa heshima za mwisho katika mwili wa Waziri Mkuu mstaafu Hayati Edward Lowassa katika kijiji cha Ngarash, Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha jana. PICHA: GETRUDE MPEZYA 

Mambo hayo ni yale aliyoyafanya kiongozi huyo ambaye Jumamosi iliyopita alihitimisha safari yake ya maisha baada ya kuaga dunia katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dar es Salaam. 

Lowassa ambaye alishika nyadhifa mbalimbali ndani ya serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo anapumzishwa rasmi nyumbani kwao, Monduli mkoani Arusha katika maziko yanayotarajiwa kuongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Miongoni mwa nyadhifa alizowahi kushika serikalini ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu; Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi; Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira); Waziri wa Maji na Mifugo; na Waziri Mkuu. Katika utumishi wa umma, aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).

 Lowassa ambaye kwa mujibu wa watu wa karibu nyota yake ya uongozi ilianza kuonekana tangu alipokuwa shule ya msingi, ameacha alama au mambo ambayo yatamfanya akumbukwe.

Miongoni mwa mambo hayo, yalitajwa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati akitoa hoja ya kuahirisha shughuli za Bunge huku akibainisha kuwa Lowassa ataendelea kukumbukwa kwa rekodi kubwa ya kusimamia mambo yenye maslahi mapana kwa taifa.

USAFIRI BODABODAMiongoni mwa mambo ambayo ni kikwazo katika kufanikisha shughuli mbalimbali ni usafiri hasa katika miji mikubwa ikiwamo Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Dodoma na Mbeya. Changamoto hiyo imewafanya watu wengi kushindwa kufika maeneo ya kazi na kurejea kwa wakati nyumbani baada ya kazi. 

Kwa kutambua hilo, Majaliwa alisema Lowassa, enzi za uhai wake, ndiye aliyeruhusu biashara ya pikipiki kubeba abiria, hatua ambayo ilisaidia vijana wengi nchini kupata ajira.

VYUO VYA UALIMU Majaliwa alisema mchango wa Lowassa aliyekuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Nne, ni pamoja na kusimamia uamuzi wa serikali kubadili vilivyokuwa vyuo vya ualimu vya Mkwawa na Chang’ombe kuwa vyuo vikuu vishiriki vya elimu. 

ZAHANATI, VITUO VYA AFYAJambo lingine kwa mujibu wa Majaliwa, ni ujenzi wa zahanati na vituo vya afya katika ngazi za vijiji na kata. 

Lowasa alihimiza ujenzi wa vituo hivyo vya kutolea huduma za afya akiwa Waziri Mkuu kutokana na serikali kuanzisha Mpango wa maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM). Kupitia mpango huo, kila kijiji kinapaswa kuwa na zahanati huku kila kata kuwa na kituo cha afya. 

USIMAMIZI MMES Baada ya mafanikio makubwa katika Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM), serikali ya awamu ya nne ilianzisha mpango kama huo kwa elimu ya sekondari (MMES). Katika mpango huo, ilisisitizwa kuwe na angalau shule ya sekondari katika kila kata. 

Lowassa akiwa Waziri Mkuu, alisimamia ujenzi wa shule hizo, maarufu kama sekondari za kata na ndani ya uongozi wake akiwa Waziri Mkuu, ilishuhudiwa kasi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vilivyochochea vijana wengi wa kitanzania waliomaliza elimu ya msingi kujiunga na sekondari. 

WAFUGAJI KUSOMA Jamii ya wafugaji wa kabila la Wamasai kwa miaka mingi imekuwa nyuma katika suala la elimu kutokana na utamaduni wa kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa ajili ya kutafuta malisho ya mifugo. 

Kutokana na hali hiyo, Lowassa alikuwa mstari wa mbele kuhamasisha jamii ya wafugaji kupenda elimu kwa kuanzisha shule nyingi za sekondari katika maeneo yao, kutilia mkazo suala la elimu na kupiga vita mimba kwa wanafunzi pamoja na kuolewa wangali wadogo.

UTATUZI KERO BALOZIKwa mujibu wa Majaliwa, Lowassa akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya  Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, alifanikiwa kutatua changamoto za baadhi ya ofisi za balozi za Tanzania kuchelewa kupata mawasiliano, hususan pale balozi anapohitimisha muda wake.

“Alihakikisha kunakuwapo mawasiliano ya haraka pamoja na kutatua suala la ‘diplomatic bags’ kutoa majibu kwa haraka. Vilevile, Kamati hiyo ilianzisha utaratibu wa kutembelea ofisi za balozi zetu katika nchi mbalimbali, jambo ambalo lilisaidia kubaini changamoto na kuzitafutia ufumbuzi,” alisema Majaliwa.

Hata hivyo, Nipashe katika uchambuzi wake limebaini kuna baadhi ya mambo ambayo Lowassa aliyafanya ama kushiriki ambayo yameacha alama hadi sasa.

MAJI ZIWA VICTORIASuala la matumizi ya maji ya Ziwa Victoria yamekuwa ya vuta nikuvute kwa miaka mingi. Akiwa Waziri wa Maji katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Lowassa alianzisha hoja na kufanikiwa kulishawishi Baraza la Mawaziri kukubali mpango wa kutoa maji katika Ziwa Victoria na kuyapeleka kwa wananchi wa mikoa ya Mwanza na Shinyanga.

Kabla ya kufanikisha azma hiyo, alikutana na ugumu kwenye mradi huo kutokana na mkataba wa zamani wa kimataifa kuipa Misri haki ya kumiliki Ziwa Victoria kwa sababu ya Mto Nile kuwa tegemeo la nchi hiyo.

WALIMU ‘VODA FASTA’Kutokana na kasi ya ujenzi wa shule za sekondari za kata na ongezeko la wanafunzi, kuliibuka upungufu wa walimu katika shule hizo. Hatua hiyo ilimfanya Lowassa akiwa Waziri Mkuu kuibuka na Mpango Maalum wa Kuendeleza Walimu (Crash Program) ili kukabiliana nao ambao ulibatizwa kama ‘Voda Fasta’.

UTATUZI MIGOGORO YA ARDHIAkiwa Waziri wa Ardhi, Lowassa alitatua migogoro sugu ya ardhi ya wawekezaji na wananchi waliokuwa wakigombea mashamba makubwa ya Valeska, mashamba ya maua ya Kiliflora lililoko USA-River, Kiliflora Nduruma na Blooms Chekereni.

UTHUBUTU Wahenga wanasema ukitaka kufanikiwa ni sharti kuwa na uthubutu. Lowassa alikuwa mtu wa kuthubutu kutenda kila alichoamini kinawezekana na ndiyo maana watu wengi wamemwelezea kuwa hakuwa mtu wa kusitasita katika yale aliyokuwa anayapanga. Alikuwa akitekeleza. 

UFUATILIAJI Licha ya uthubutu, Lowassa alikuwa mtu wa kufuatilia mambo katika sekta alizokuwa akiziongoza ikiwamo alipokuwa Waziri Mkuu. Hatua hiyo ya ufuatiliaji ilimfanya awe mtu wa kutumia maneno ‘naagiza’, nataka’,  na ‘naelekeza’  badala ya neno ‘naomba’.   

KUCHUKIA UMASKINI Lowassa katika maisha yake alikuwa mtu wa kuchukia umaskini kwa vitendo. Kutokana na dhamira hiyo, alikuwa mchapakazi akiamini kuwa kazi ndiyo msingi wa kufanikiwa katika kila jambo.   

KUJALI WANANCHIMaendeleo ndani ya Monduli yana mkono wa Lowassa hali inayodhihirisha kuwa alikuwa akijali wananchi na kushiriki kutatua shida na matatizo yaliyokuwa yakiwakabili