Mama adaiwa kuua wanawe wawili kwa soda yenye sumu

11Mar 2024
Nebart Msokwa
MBEYA
Nipashe
Mama adaiwa kuua wanawe wawili kwa soda yenye sumu

​​​​​​​JESHI la Polisi mkoani Mbeya linamshikilia Dainess Mwashambo (30), mkazi wa Kijiji cha Mashesye, Kata ya Ilungu, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kwa tuhuma za kuua watoto wake wawili kwa kuwanywesha sumu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Benjamin Kuzaga.

Inadaiwa kuwa baada ya kutekeleza unyama huo, mama huyo alifanya jaribio la kujiua kwa kunywa sumu hiyo ili kukwepa mkono wa sheria.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Benjamin Kuzaga amesema kuwa mtuhumiwa huyo aliwaua watoto hao kwa kutumia dawa ya kukaushia majani shambani ijulikanayo kwa jina la Pare Force.

Ametaja watoto waliofariki dunia ni Mario Adamson (4) na mdogo wake wa kike, Beonis Adamson (2. Wote walifariki wakati wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Mbeya.

Kamanda Kuzaga amesema chanzo cha tukio hilo ni msongo wa mawazo uliosababishwa na mwanamke huyo kutuhumiwa na serikali ya kijiji hicho kwa wizi, pia aibu iliyotokana na tukio hilo.

Kamanda Kuzaga amesema kuwa Machi 3, mwaka huu, mtuhumiwa alidaiwa kuingia kwenye nyumba ya mwanakijiji mwenzake, Zaria Ndagwa kwa nia ya kuiba vitu ambavyo havikutajwa.

Amesema kuwa mtuhumiwa alikutwa na mwanakijiji mwingine aitwaye Asnat Mapayo ambaye alitoa taarifa kwa mwenye nyumba na ndipo akashtakiwa kwenye serikali ya kijiji.

Amesema kuwa Machi 6, mwaka huu, mama huyo aliitwa na viongozi wa serikali ya kijiji kwa lengo la kumhoji na alikiri kufanya kosa hilo na ndipo wakamtoza faini ya Sh. 25,000 kwa ajili ya gharama za uendeshaji kesi na Sh. 100,000 kama fidia kwa mwenye nyumba alimotaka kuiba.

Amesema mama huyo aliomba viongozi wa serikali ya kijiji hicho apunguziwe adhabu hiyo ili badala ya kulipa Sh. 125,000 alipe Sh. 50,000 pekee, faini ambayo ilikubaliwa na akaambiwa akaitafute.

“Ilipofika Machi 7, mwaka huu, ndipo ikabainika kuwa alikuwa amewanywesha sumu watoto wake kwa kuichanganya kwenye soda na na yeye mwenyewe akawa amekunywa ndipo zikaanza jitihada za kuokoa maisha yao kwa kuwakimbiza hospitalini,” amesema Kamanda Kuzaga.

Amesema watoto hao walifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa katika hospitali hiyo ya rufani na kwamba mama huyo anaendelea na matibabu katika hospitali hiyo akiwa chini ya ulinzi.

Kamanda huyo amewataka wananchi mkoani Mbeya kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwa kuwa inasababisha madhara hata kwa watu wasiokuwa na hatia kama ambavyo mwanamke huyo amewaua watoto wake.

Ameshauri wananchi wanaopata tatizo la kifamilia, kupata msaada kwa jeshi hilo kupitia dawati la jinsia na watoto au kwa viongozi wa serikali wakiwamo maofisa ustawi wa jamii.

Kamanda Kuzaga amesema mtuhumiwa huyo baada ya kutibiwa na kupona, atachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.