Maji yatajwa kuua 14 Shinyanga

04Mar 2024
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Maji yatajwa kuua 14 Shinyanga

​​​​​​​KATI ya vifo 24 vilivyotokana na matukio mbalimbali mkoani Shinyanga kwa mwaka 2023, 14 vimetajwa kutokana na watu kusombwa na maji.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Shinyanga, Martin Nyambala, amebainisha hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kutoa taarifa ya matukio yaliyotokea mwaka jana.

Amesema kwa kipindi hicho yalitokea matukio yasiyozidi 80, ambako kati ya hayo matukio ya moto majumbani yalikuwa 29, taasisi na biashara 18, miundombinu ya umeme 10, ajali barabarani saba na ajali za maji 13.

Ametaja vifo vilivyotokea kufuatia matukio hayo kuwa ni 24 huku majeruhi wakiwa 41 ambako kati ya vifo hivyo 24, 14 vilitokana na watu kusombwa na maji 14 kwenye mito.

"Wengine watano walifariki dunia kwa ajali ya moto na waliosalia watano walifariki dunia katika matukio mengine zikiwamo ajali za barabarani,” amesema Nyambala.

Ametoa wito kwa wananchi kuwa makini na mvua ambazo zinaendelea kunyesha kwa kutovuka kwenye mito iliyojaa maji na kuzuia pia watoto wao wasiende kuogelea wala kuvua samaki kwenye mito hiyo.

Ametahadharisha pia wakazi wanaioshi mabondeni na kwenye mikondo ya maji wahame ili kunusuru maisha yao.

Katika hatua nyingine, Nyambala ametaka wananchi kuwa makini na matumizi ya nishati majumbani ikiwamo gesi pamoja na jiko mkaa, kwamba wanapopikia ndani wahakikishe madirisha yanakuwa wazi, ili kupitisha hewa na kuwa salama wakati wa matumizi.

Ameelekeza wafanyabiashara kuhakikisha wana vifaa vya kuzimia moto ili waudhibiti unapoanza kuwaka wakati Jeshi hilo likiwa njiani kuwaongezea nguvu ili kunusuru vitu na watu.

Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Shinyanga, wameliomba jeshi hilo kuwa na utaratibu wa kutoa elimu mara kwa mara kwa wananchi, namna ya kuepukana na majanga ya moto ambayo yanatokana na uzembe, pamoja na jinsi ya kuuzima moto kwa hatua za awali.