Majaliwa amesema utabiri wa wataalamu wa hali ya hewa nchini unaonyesha kuwa kutakuwa na mvua kubwa inayoweza kusababisha maafa kwa watu wa mabondeni, hivyo hawana budi kuondoka wenyewe.
Waziri Mkuu alitoa tahadhari hiyo jana jijini Dar es Salaam katika mkutano ulioandaliwa na Jukwaa la Wadau wa Maendeleo la mikoa ya Rukwa na Katavi, ili kutathmini maendeleo ya mwaka 2000-2025 kwa mikoa hiyo.
Hadi sasa nyumba zaidi ya 600 zimekwishabomolewa katika Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, huku Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Ardhi ikisitisha kuendelea kwa bomoabomoa ya nyumba zilizoko mabondeni.
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Ardhi imesitisha bomoabomoa kupisha kesi ya msingi iliyofunguliwa kwa msaada wa mbunge wa jimbo hilo, Maulid Mtulia (CUF).
Wakazi 600 wa bonde la Mto Msimbazi wanapinga bomoabomoa ya zaidi ya nyumba 15,000 zinazotarajiwa kubomolewa katika maeneo mbalimbali ya mabondeni.
Bomoabomoa hiyo ilianza Desemba 17 mwaka jana, kisha kusitishwa kwa siku 14 kupisha wananchi kujiandaa kwa kubomoa zaidi ya nyumba 300, ambazo zimefikia jumla nyumba 600.
Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa alisisitiza kusimamiwa kikamilifu kwa masuala mbalimbali katika sekta ya elimu, afya, miundombinu na ufugaji na kwamba masuala hayo yanahitaji kutekelezwa na wakuu wa mikoa pamoja na wilaya nchini.
“Wakuu wa mikoa, wilaya wasimamie suala la ufugaji wa kisasa ambao utapunguza migogoro ya wafugaji, kilimo kisimamiwe ili kuzalisha ziada, pamoja na suala la elimu bure muhakikishe kila shule inakuwa na madawati ya kutosha,” alisema Majaliwa.
Alisema serikali inaendelea kusisitiza kila Mtanzania kulipa kodi, ili kuongeza fedha za kukamilisha miradi ya maendeleo nchini.
“Serikali ya awamu ya tano haina nia ya kumkomoa mtu katika suala la kulipa kodi, bali tunamkumbusha kila mtu wajibu wake, ili rasilimali fedha ipatikane kwa maendeleo ya miradi tuliyokwishaanza,” alisema.










