Hatua hiyo ni kutokana na madai ya utendaji wake kutoridhisha ikiwamo kutochukua hatua kwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa iliyoko Bukoba, iliyozuia maiti ya mtoto mchanga.
Wakati akiagiza hatua hizo kuchukuliwa, Mchengerwa ameapa kuwashughulikia viongozi wa kisiasa na serikali ambao wamekuwa chanzo cha kukwamisha miradi ya maendeleo na kutishia kusitisha vikao vya Baraza la Madiwani Manispaa ya Bukoba iwapo litabainika kikwazo kwa maendeleo.
Alisema hayo katika hafla ya utiaji saini mikataba ya usanifu wa miradi ya uboreshaji miundombinu ya miji ya Tanzania (TACTIC) kwa miji 15 ya kundi la pili mjini hapa.
“Nimepata taarifa moja ya hospitali zetu mtoto amefariki dunia wamekaa zaidi ya siku mbili hawataki kuachia maiti ya mtoto mchanga huku wakijua anapaswa kuhudumiwa bure na maiti yake anapofariki aruhusiwe kwenda kuzikwa. Utoaji wa huduma lugha mbovu umeenea katika hospitali ya mkoa. Hili sitakubali hata kidogo. Nakuelekeza Katibu Mkuu kutengua mara moja nafasi ya mganga mkuu wa mkoa,” alisema huku akisisitiza kuwa ni dhamana, mtu akishindwa kuwahudumia Watanzania hafai kwenye nafasi na ataondolewa.
Kuhusu maendeleo ya Bukoba, alisema kuna maeneo hawafanyi vizuri kwenye miradi kwa sababu kuna viongozi wa serikali wanaweka mikono yao.
“Viongozi wengine wanaweka mkono, wanatafuta makandarasi wao, miradi inakwama na haijengwi inavyotakiwa. Sasa nataka niwaambie wazi kiongozi yeyote wa serikali anayewajibika chini ya TAMISEMI atakayeweka mkono kwenye miradi hii ambayo Rais anataka kuwakwamua wananchi, nitashughulika naye.
“Bukoba imefika hapa ilipo kwa sababu kuna watu hawatamani kuona maendeleo kwa sababu ya maslahi yao ya kisiasa, tena wengine viongozi ndani ya serikali,” alisema huku akiapa kuwa katika utekelezaji wa miradi hiyo, hatakubali kufumbia macho yeyote atakayethubutu kuikwamisha.
Alisema soko na stendi mkoani Kagera ni miundombinu ya muda mrefu tangu vita vya Kagera mwaka 1978/79 lakini sasa itajengwa ya kisasa.
Mchengerwa alisema Rais Samia Suluhu Hassan amemfuta machozi Mbunge wa Bukoba Mjini, Stephen Byabato, ambaye hivi karibuni alipiga magoti na kuangua kilio akiomba ujenzi wa miradi ya soko, stendi, barabara na kujenga kingo kwenye Mto Kanoni ili kuondokana na kero ya mafuriko.
MIRADI KUWANG’OA MA-DED
Mchengerwa alisema mkurugenzi wa halmashauri atakayeshindwa kukamilisha kwa muda uliopangwa ujenzi wa shule kupitia fedha za BOOST na SEQUIP ifikapo Desemba 31, mwaka huu, atapendekezwa kwa Rais aondolewe kwenye nafasi yake.
“Nendeni mkasimamie miradi fedha zimetolewa, sitegemei kusikia kuna mkurugenzi ambaye ameshindwa kutekeleza miradi katika maeneo yake,” alisema.
Akitoa maelezo ya mradi wa TACTIC, Mratibu wa Miradi ya Ushirikiano wa Benki ya Dunia na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), Mhandisi Humphrey Kanyenye, alisema mradi unagharamiwa na serikali kuu kwa Sh. trilioni moja kupitia masharti ya nafuu ya mkopo kutoka Benki ya Dunia na utanufaisha miji 45.
“Mradi utatekelezwa kwa miaka sita kuanzia mwaka wa fedha 2022/23 lengo kuu ni kuboresha usimamizi wa ukuaji wa miji pamoja na kuwezesha halmashauri za miji na majiji kutoa huduma bora kwa wananchi. Maeneo ya utekelezaji ni ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwamo barabara na miundombinu mingine kulingana na vipaumbele vya halmashauri husika,” alisema.
Alisema kundi la kwanza linahusisha miji 12 ya Mwanza, Mbeya, Arusha, Dodoma, Morogoro, Kahama, Kigoma, Songea, Sumbawanga, Tabora, Geita na utekelezaji wake umeanza mwaka huu wa fedha 2023/24.
Kundi la pili, alisema litahusisha miji 15 ya Tanga, Korogwe, Moshi, Kibaha, Iringa, Bukoba, Singida, Bariadi, Shinyanga, Musoma, Lindi, Mpanda, Njombe, Mtwara na Babati na utekelezaji wake utaanza mwaka ujao wa fedha 2024/25 baada ya usanifu kukamilika.
“Kundi la tatu linahusisha Miji 18 ya Kasulu, Tunduma, Vwawa, Ifaraka, Masasi, Nanyamba, Handeni, Bagamoyo, Mafinga, Tarime, Chato, Bunda, Mbinga,Mbulu, Nzega, Kondoa, Newala ambao utekelezaji utaanza mwaka 2024/25,”alisema.









