Magufuli ataka mawaziri wajiandae kwa machungu

17Apr 2016
Beatrice Shayo
Dar
Nipashe Jumapili
Magufuli ataka mawaziri wajiandae kwa machungu
  • Wale waliozoea chai chai, semina na safari za ovyo ovyo watupishe, ataka wavumilie maana huko tuendako kutakuwa na uchungu uchungu sana..

RAIS John Magufuli amesema fedha za posho, semina na safari hazitakuwepo kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha itakayowasilishwa Bungeni mwezi ujao na kuwataka viongozi wa serikali ambao hawataweza kufanya kazi bila posho kuachia ngazi na kwenda kufanya shughuli zao binafsi.

Aidha, Rais Magufuli amewataka mawaziri, makatibu wakuu na watendaji wengine serikalini wajiandae kisaikolojia kufuatia hali ngumu ya kubana matumizi kwani watapaswa kuwa wavumilivu.

Rais Magufuli alibainisha hayo jana wakati akiweka jiwe la msingi kwenye barabara za juu (fly overs) eneo la Tazara, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari barabarani katika jiji hilo.

Barabara hizo zitajengwa na kampuni ya Sumitomo Consultants Construction Co. Ltd ya Japan. Mkataba wa ujenzi wa barabara hizo unaotarajiwa kukamilika Oktoba 2018 kwa gharima ya Sh. bilioni 100, ulisainiwa na Rais Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi katika awamu ya nne.

Akizungumza katika halfa ya jana, Rais Magufuli alisema fedha zilizokuwa zikitumika kwenye semina na safari zimeongezwa kwenye miradi ya maendeleo, ambayo bajeti yake kwenye mwaka huu wa fedha imepanda kutoka asilimia 26 hadi asilimia 40.

“Hizi fedha za chai chai, posho posho za semina na safari tumeziondoa na kuzipeleka kwenye miradi ya maendeleo," alisema Rais Magufuli na kushangiliwa kwa nguvu na umati wa wananchi uliojitokeza kushuhudia tukio hilo, kisha kutahadharisha:

"Wale waliozoea chai chai, safari za ovyo ovyo kama wanadhani hawawezi kufanya kazi bila posho hizo ni vyema wakaacha kazi.”

Aidha, Rais Magufuli alisema serikali kwenye bajeti ya mwaka huu imetenga fedha za kununua ndege tatu mpya kwasababu amechoka kuona wageni wanaokuja nchini wakishukia Kenya.

Alisema anataka kulibadili Shirika la Ndege la ATCL kuwa la kisasa zaidi, lakini alionya ili kufikia malengo hayo, watendaji wa serikali wakiwemo mawaziri na makatibu wakuu lazima wajiandae kwa machungu.

“Niwaambie kuwa watendaji itabidi mvumilie maana kutakuwa na uchungu uchungu sana huko tuendako," alisema Rais Magufuli.

"Watanzania hawa wameonja huo uchungu kwa muda mrefu sasa ni zamu yao kula utamu na nyinyi viongozi muonje uchungu.” Kauli hiyo ya Rais Magufuli ilifanya umati uliokuwepo kulipuka tena kwa shangwe.

UCHUMI WA TAIFA

Aidha, Rais Magufuli alisema mradi huo wa ujenzi wa barabara ya juu katika makutano ya Tazara, ambao utagharimu Sh. bilioni 100, tayari umetengewa Sh. bilioni 93.4.

Alisema kukamilika kwa mradi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa msongamano wa foleni kwa Jiji la Dar es Salaam na kuongeza uchumi wa taifa na wananchi mmoja mmoja.

Alisema barabara za juu zitapunguza fedha zilizokuwa zinapotea ambapo alieleza kuwa katika tafiti iliyofanywa mwaka 2013, Sh. bilioni 411.3 zilipotea katika Jiji la Dar es Salaa kutokana na msongamano.

“Ukiacha watu waliofariki dunia kwa kuchelewa kufika hospitali, kuna ndoa nyingine zilivunjika watu walichelewa kufika nyumbani wakashindwa kujitetea kwa wenzi wao,” alisema Rais Magufuli akichanganya ukweli na utani ndani yake.

Alisema mradi huo utatengeneza ajira na asilimia kubwa zitatolewa kwa watanzania, hususani kwa Dar es Salaam hivyo vijana wafanye kazi kwa uadilifu.

Aliwataka vijana ambao watapewa ajira katika mradi huo kuhakikisha wanafanya shughuli zao kwa uaminifu na kuacha mtindo wa kuiba mafuta pamoja vifaa kwani watasababishia mradi huo kukwama.

Pia alimtaka mkandarasi anayejenga barabara hiyo kuhakikisha wanamaliza ujenzi huo kabla ya Oktoba mwaka 2018 kwa kuwa wana uzoefu wa kujenga barabara kubwa nchini kwao Japani, hivyo haoni sababu ya kutumia muda mwingi.

Alisema serikali ya Japan imekuwa ikiisaidia Tanzani katika miradi mbalimbali na fedha hizo zimekuwa zikitokana na walipakodi kutoka nchini mwao. “Sh. bilioni 93.4 ni fedha za walipa kodi wa Japan, wameamua kuzileta Tanzania ambako wengine hatutaki kulipa kodi," alisema Rais Magufuli.

"Wito wangu ni kuhamasishana kulipa kodi ili miradi ya maendeleo tuweze kuitekeleza kwa fedha zetu.”

Alisema kuna barabara nyingine ya juu ambayo itajengwa yenye kilometa 128 kutoka daraja la Kigamboni hadi Chalinze ambayo itakuwa na njia sita ikiwa na barabara za juu tano na mpaka sasa zaidi ya wakandarasi 13 wamejitokeza kuwania zabuni hiyo.

Aidha, alisema kuna miradi mingine ambayo inaendelea kutelekezwa katika Jiji la Dar es Salaam.

Mbali na barabara ya juu katika makutano ya Tazara, serikali ina mpango wa kujenga njia kama hizo Ubungo kwa madhumuni hayohayo.

UFISADI UDA-DART

Wakati huo huo, Rais Magufuli alisema aliamua kuchelewesha wa mradi wa mabasi ya mwendo kasi (Uda-Dart) kwa makusudi baada ya kubaini ufisadi uliopangwa kufanywa na mmoja wa wabia wa mradi huo.

“Tulisimamisha ili hatua zote zikamilike, haiwezekani sisi tukope fedha Benki ya Dunia zaidi ya Sh. bilioni 388, halafu watokee wajanja wajanja wanaotaka kumiliki miundombinu iliyojengwa kwa jasho la watanzania,” alisema.

Alisema kwenye mradi huo, serikali ina asilimia 49 za hisa lakini walitokea watu wajanja wajanja wakitaka hisa za serikali zipotee.

Ndipo ilipoamua kuusimamisha mradi ili kurekebisha mambo, alisema Rais Magufuli.

“Tulishtuka tukasema haiwezekani, hakuna kitu kama hicho, sasa mambo yamekwenda vizuri na nataka niwahakikishie mradi huu utaanza maana tuliuchelewa kwa ajili ya kulinda manufaa ya watanzania.

"Haiwezeakani tukope fedha halafu atokee mtu mmoja apewe mamlaka ya kutumia hii barabara peke yake, huu ni ufisadi wa ajabu.”

Alisema kuna njama zilifanyika kutaka kuifanya nauli ya mabasi hayo kuwa ya juu kuliko ya daladala lakini serikali yake ilishtuka tena na kuingilia kati kwa kuishusha ili wananchi waimudu.

AHIMIZA USAFI

Aidha, Rais Magufuli alimuagizi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuhakikisha jiji linakuwa katika hali ya usafi kwa kuwa ni kitovu cha Tanzania na kwamba mradi huo hautakuwa wa maana kama likiendelea kuwa chafu.

“Dar es Salaam mpya inakuja, anayetupa uchafu apigwe faini kubwa na yule anayemkamata apatiwe hata asilimia 80 ya fedha inayotozwa," alisema Rais Magufuli.

"Haiwezekani Kilimanjaro wanaogopa kutupa taka ovyo alafu wakija Dar es Salaam wanatupa ovyo.”

Naye Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, alisema ujenzi wa barabara hiyo ulitakiwa kuanza tangu mwaka 2013 na kwamba ucheleweshaji umetokana na kukosekana kwa mkandarasi.

Alisema wakandarasi ambao walikuwa wakipatikana walikuwa na gharama kubwa ikilinganishwa na fedha zilizotengwa. “Ilitubidi tuongeze gharama hadi kufikia bilioni 93.4 ndipo tulipowatafuta wakandarasi wawili na mmoja ndio huyo aliyekubalia kuanza ujenzi ambaye ni Sumitomo Consultants Construction Co. Ltd,” alisema Profesa Mbarawa.

Naye Mwakilishi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa (JICA), Toshio Nagase, alisema ujenzi wa barabara hiyo ni kumbukumbu ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Japan.

Alisema barabara hiyo itachangia katika kuboresha maisha ya wananchi wa Dar es Salaam na ukuaji wa uchumi wa Tanzania na kuahidi kujenga mradi huo kwa kuzingatia kiwango bora.

Naye Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida, alisema wameshukuru kwa maandalizi mazuri ya mradi huo na kwamba serikali yake itaendelea kuwa washiriki wa maendeleo.