Mabasi yapeleka LATRA ombi kupandisha nauli

15Oct 2023
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Mabasi yapeleka LATRA ombi kupandisha nauli

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imepokea maombi kutoka kampuni tatu zinazotoa huduma ya usafiri wa abiria wa masafa marefu kufanya marejeo ya nauli za mabasi kutokana na ongezeko la gharama za uendeshaji.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano cha  LATRA, kampuni hizo ni Super Feo Enterprises, ABC Upper Class and Transportation Ltd na Happy Nation Co. Ltd.

Taarifa hiyo ilisema kuwa kampuni hizo zimeomba LATRA kufanya marejeo ya nauli za mabasi huku zikitaja sababu nyingine kuwa ni kupanda kwa bei ya mafuta (petroli na dizeli).

“Mapendekezo ya kampuni hizo ni kuongeza nauli ya sasa ya Sh. 56.88 kwa kilometa moja kwa kila abiria. Super Feo Enterprises kwa daraja la kati nauli pendekezwa kwa kilometa moja kwa kila abiria imeomba iwe Sh. 101.88 na ongezeko kwa kilometa moja kwa kila abiria iwe Sh. 45 sawa na asilimia 79.11,” ilisema.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa ABC Upper Class and Transportation imependekeza kwa daraja la kati nauli kwa kilometa moja kwa kila abiria iwe Sh. 92.84 ongezeko kwa kilometa moja kwa kila abiria iwe Sh. 36.96 sawa na asilimia 63.22.

Aidha, ilisema Happy Nation Co. Ltd kwa daraja la kati nauli pendekezwa kwa kilometa moja kwa kila abiria ni 84.06 na ongezeko kwa kilometa moja kwa kila abiria Sh. 27.18 sawa na 47.78.

“Kwa kuzingatia kifungu cha 21 cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura ya 413 pamoja na kanuni ya 9(3) ya Kanuni za LATRA (Tozo) za Mwaka 2020 (Tangazo la Serikali Na. 82 la tarehe 7/2/2020), mamlaka inapaswa kutoa fursa kwa kampuni hizi kuwasilisha mapendekezo yao kwa wadau wa usafiri wa abiria kisha kukusanya maoni ya wadau kabla ya kufikia uamuzi wa kufanya marejeo ya nauli zilizotumika,” ilisema taarifa hiyo.

Pia taarifa ilisema nauli zinazotumika kwa sasa zilitangazwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 18 la tarehe 6 Mei, 2022.

Taarifa hiyo ilisema kutokana na maombi hayo, mamlaka imeandaa mkutano wa wadau kupokea maoni utakaofanyika Oktoba 18, mwaka huu, katika ukumbi wa Arnaoutouglou, Dar es Salaam kuanzia saa 3:00 asubuhi.

Aidha, taarifa ilisema LATRA itawasilisha mapendekezo ya vigezo vya mchakato wa kuridhia mapitio ya viwango vya nauli za mabasi yanayotoa huduma mijini (daladala). “Wasilisho la LATRA litafanywa kwa mujibu wa kanuni ya 13 ya Kanuni za LATRA (Tozo) za Mwaka 2020 (Tangazo la Serikali. Na. 82 la tarehe 7/2/2020).

“Kutokana na umuhimu wa suala hili, LATRA inawaalika wadau wote wa usafiri wa umma na wananchi kwa ujumla kuhudhuria mkutano huu muhimu ili kutoa maoni baada ya kusikiliza mapendekezo yatakayowasilishwa na kampuni zilizoleta maombi ,” ilisema.