M500/- kuboresha mazingira Dar

06Feb 2016
Romana Mallya
Nipashe
M500/- kuboresha mazingira Dar

HALMASHAURI ya jiji la Dar es Salaam itatumia Sh. Milioni 500 kutekeleza mpango wa kuboresha huduma za usafi wa mazingira ulioandaliwa na Serikali za Mitaa mkoani humo.

Mkuu wa Kitengo cha Itifaki na Uhusiano na Umma wa Halmashauri hiyo, Gaston Makwembe, aliyasema hayo jana na kusisitiza kuwa, utekelezaji utakapoanza biashara zisizo rasmi, bodaboda, guta na mikokoteni haitaruhusiwa katika eneo maalum litakalojulikana kama ‘Smart Area’.
Pia alisema majengo chakavu na mabovu yatabomolewa, utupaji taka ovyo na matumizi ya maeneo yasiyo rasmi kwa ajili ya kukusanyia taka yatadhibitiwa kwa kufuata na kusimamia sheria.
Aidha, Makwembe alisema mambo mengine yasiyohitajika katika eneo hilo ni ombaomba, wamachinga kufanya biashara za mikononi na wale waliosajiliwa hawataruhusiwa kupanga biashara nje ya maduka yao.
Alitaja mambo mengine yasiyoruhusiwa kuwa ni kuwasha moto na kupika katika maeneo yasiyo rasmi, gereji bubu za magari katika makazi ya watu, uegeshaji ovyo magari, kujisaidia na kutema mate ovyo.
Nyingine ni mabango yaliyochakaa kwenye vituo vya mabasi, nyumba au majengo kutumiwa bila kuwa na ‘pavements’ zilizojengwa kitaalam.
Pia alisema haitaruhusiwa kubandika matangazo bila kibali maalum, kuunganisha mfumo wa maji taka wenye mifereji ya wazi ya maji ya mvua ni sehemu ya shughuli zinazozuiliwa.
“Uoshaji wa magari katika maeneo yasiyo rasmi katika eneo la smart area, kusababisha kelele na kupiga muziki kwa sauti kubwa bila kupata kibali pamoja na kuingiza malori zaidi ya tani 10 bila kibali ni shughuli zilizopigwa marufuku,” alisema.
Akifafanua kuhusu ‘smart Area’, Makwembe alisema linaundwa na manispaa zote tatu ambazo ni Ilala, Kinondoni na Temeke na tayari limekwishaainishwa.
Alisema utekelezaji huo utasimamiwa na mkurugenzi wa jiji na kuratibiwa na katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam.
Alitaja maeneo yatakayohusishwa kuwa ni kuanzia makutano ya barabara ya Uhuru na Kawawa hadi Morocco.
Mengine ni barabara ya Ali Hassani Mwinyi kuanzia eneo la Morocco hadi daraja la Selander kuelekea fukwe za Ocean Road, Kivukoni, Bandari hadi makutano ya barabara ya Kilwa na Mandela (eneo la uhasibu) na ile ya Nyerere na Mandela (eneo la Tazara).
Mengine ni kuanzia makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela (eneo la Tazara) hadi makutano ya barabara ya Kawawa na Uhuru.
Alitaja maeneo ya kiutalii kuwa ni yale yote ya fukwe huku njia kuu za mapokezi ya wageni kuwa ni barabara ya Nyerere kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, barabara ya Mwai Kibaki hadi hoteli ya Whitesands kupitia ile ya Mbezi chini.
Nyingine ni barabara ya Morogoro na zile zote za Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka.