Lissu azuiwa redioni, Nape amtetea

08Feb 2024
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Lissu azuiwa redioni, Nape amtetea

​​​​​​​KUMEIBUKA utata kuhusu kuahirishwa kwa mahojiano kati ya Tundu Lissu na watangazaji wa Wasafi Media, mwenyewe akifunga safari hadi kwenye studio za chombo hicho cha habari jijini Dar es Salaam akitaka aelezwe nani aliyetoa agizo la zuio hilo.

Kukiwa na utata huo, serikali kupitia Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, imesema haihusiki na kuzuiliwa kwa mahojiano hayo yaliyopangwa kufanyika jana kwenye Kituo cha Redio cha Wasafi FM.

Jana asubuhi, kulisambazwa taarifa kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii kuwa Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alifika kwenye studio za Wasafi FM akitaka apewe sababu kwanini kipindi chake kilizuiliwa kufanyika.

Katika kipande kifupi cha video kilichosambazwa jana kwenye mitandao hiyo, kilionesha watangazaji wa kituo hicho wakithibitisha walikuwa na ratiba ya mazungumzo na Lissu, lakini kutokana na kwa sababu zilizo nje ya uwezo wao, kiliondolewa.

"Jana (juzi) hapa tulikuwa tumekubaliana tungekuwa na Tundu Lissu, lakini kwa bahati mbaya sana, kwa sababu ambazo ziko nje kabisa ya uwezo wetu, ile ‘interview’ (mahojiano) ikawa imekuwa ‘cancelled’ (imefutwa) jana (juzi) jioni kabisa.

"Lakini Tundu Lissu mwenyewe kwa bahati mbaya alisema hakuridhika na hakupata sababu za kutosha," alidai mmoja wa watangazaji wa kiume wa kituo hicho.

Ilidaiwa kuwa Lissu alifika katika ofisi za chombo cha habari hicho saa 10 alfajiri na akakaa kwa zaidi ya saa tatu, akisubiri kupatiwa sababu za kuzuiwa kwa mazungumzo yao redioni.

Baadaye Lissu alifanikiwa kufanya mazungumzo na uongozi wa kituo hicho na akaweka wazi baadhi ya waliyozungumza ofisini.

"Nilipopata mwaliko ule, nilikuwa na wasiwasi kidogo kwa sababu ninafahamu kwamba masuala ya vyombo vyetu vya habari yamekuwa na matatizo kwa miaka kadhaa sasa.

"Kwahiyo, nilikuwa na shaka kwamba kweli hawa wataweza kukubali nije kwenye kipindi chao? Lakini walinitoa hiyo shaka kwamba 'tumezungumza na wakubwa wetu, mambo yote yako sawa, Mheshimiwa usiache kuja'.

"Jana (juzi) usiku, nikapata habari kwamba kipindi kimechomolewa (mahojiano yao yamefutwa). Nikauliza 'kwanini?' Jibu nililopewa ni 'maagizo kutoka juu'.

"Nikasema 'nitakuja asubuhi na mapema kuja kuuliza ili nithibitishiwe kama yale mambo ya maagizo kutoka juu tuliyokuwa tunafikiria bado yapo'. Kwahiyo, ndicho kilichonileta hapa," Lissu alisema.

Msomi huyo wa sheria alisema kuwa baada ya kuzungumza na uongozi wa kituo hicho, aliridhika pasi na shaka na sababu alizopewa.

"Nimezungumza na viongozi wa Wasafi TV, wamenihakikishia kwamba kipindi hakijachomolewa kwa sababu ya maagizo kutoka juu, bali kulikuwa na matatizo ya mawasiliano miongoni mwa waandaaji wa kipindi pamoja na menejimenti kwa namna ambayo kipindi kisingekuwa bora.

"Na nilivyopata hayo maelezo nimewaambia, na ninaomba niiseme hii kwamba sina sababu yoyote ya kutokuwaamini, kutokuamini maneno yao.

"Wamesema ni kwa sababu ya hayo mawasiliano kutokuwa sawa miongoni mwao si kwa sababu za maagizo kutoka juu na tumekubaliana kwamba tutafute muda mwafaka wafanye maandalizi wanayoona yanastahili ili nije kufanya kipindi katika siku zijazo. Ndicho ambacho ningependa kukisema kwa hatua ya sasa," Lissu alisema.

KAULI YA WIZARA

Katika tamko lake la jana jijini Dodoma kuhusu suala hilo, Nape mbali na kusema serikali haihusiki na kilichojiri, aliutaka uongozi wa Wasafi Media useme ukweli kuhusu kilichotokea mpaka mahojiano hayo kutofanywa.

Waziri huyo alisema kuwa tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani (Machi 19, 2021), serikali imefanya mambo mengi mazuri kwa tasnia ya habari, ikiwa ni pamoja na kufungulia vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungwa na kutoa maelekezo kwa Wizara ya Habari kuhakikisha kunakuwa na uhuru wa vyombo vya habari nchini.

"Rais pia amehakikisha kuwapo demokrasia nchini ikiwamo uhuru wa watu wote kuzungumza bila kuzuiwa, wakiwamo viongozi wa vyama vyote vya siasa  na aliagiza kuangalia ustawi wa vyombo vya habari kiuchumi na kuandaa kamati ya kutathmini hali ya uchumi wa vyombo hivyo.

"Kutokana na nia yake hiyo njema ya Rais, hakuna uwezekano wa maelekezo yoyote ya kuingilia uhuru ambao amekuwa akiamini na kuujenga kwa vyombo vya habari nchini," alisema.

Waziri Nape pia alisema serikali imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha uhuru wa vyombo vya habari kama dira yake ya kuendeleza dhana yake nzima ya 'Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Utaifa, yaani 4R)'.

Alisema serikali itaendelea kulinda uhuru wa vyombo vya habari na akavitaka vyombo hivyo kutoa nafasi kwa vyama vyote vya siasa bila upendeleo hasa wakati huu kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2025.