“Haikuwa kazi nyepesi kwangu kuingia baharini peke yangu mwanamke na kuwa Nahodha na kuchukua chombo na kuanza kuzunguka nacho baharini, bila ya mwanaume,” anatamka Nahodha wa chombo cha majini, Bahati Issa (51).
Anaendelea: “Lakini kwa sababu wanawake huwa tunaamini hakuna tusichokiweza na tukiamua jambo, huwa tunalikamia sana, ili basi na mimi nikasema nitaweza na nikaingia mzigoni.”
Bahati anaisimulia Nipashe, akiwa katika Pwani ya Unguja, kwamba wasifu wake kifamilia ni mama wa watoto sita, ameolewa na mume Khamis Hassan Haji, kazini akiendesha chombo cha baharini kiitwacho Nipe Tano, jina linalobeba tafsiri hitaji la kuungwa mkono.
Bahati anaangukia orodha ya wanawake walio na uthubutu wa kusafirisha watalii kutoka endo maarufu kijiji cha Kikungwi, mkoa wa Kusini Unguja
Akiwa na boti yenye mashine ya kisasa kutoka, wakisafiri hadi katika visiwa maalum vyenye uwekezaji mkubwa, ikiwamo Nyemembe, Miwi, Komonda, Kwale na Punguze.
Ni safari za visiwani zinazochukua mwendo baharini wastani wa dakika 30 hadi dakika 60, kutegemea na umbali wa killipo na huwa anajikita huko, akitumikia unahodha wake.
Anataja siri ya kuhama kitaaluma eneo hilo, ni kwamba, baada ya kuona wanaume wamejikita peke yao katika kazi hiyo, akitaja sababu kwamba:.
“Baada ya kuona shughuli hizi zinafanywa na wanaume peke yao kijijini hapa, wakati wanawake na sisi tuna fursa ya kufanya kazi hii.
“Na baada ya kuingia nimekubalika na nimeaminika maana baadhi ya watalii hawaridhiki mpaka niwasafirishe mimi na wamenipachika jina la Mama Afrika,” anasimulia.
Bahati anasema,baada ya kuwafikisha watalii visiwani, pia anawahudumia kwa kuwaandalia chakula, ambapo kawaida baada ya kuogolea, huhitaji mlo kabla ya kuwarudisha katika eneo la awali.
Akieleza mafanikio aliyoyapata kutokana na kazi hiyo, amemudu kujenga nyumba ya makazi anakoishi, anawasomesha watoto wake shule, pia amenunua chombo cha usafiri bodaboda kwa ajili ya biashara.
Sasa bahati anatoa rai, kwamba wanawake wenzake kujitoa bila ya kuchagua kazi na upungufu wa kijinsia iwe pingamizi ya wanawake kufanya kazi za kujikwamua kiuchumi na kupata kipato.
ALIKOKUWA ZAMANI
Anataja awali kabla ya kazi hiyo ya unahodha, alijishughulisha na a uvuvi wa chaza akiwa na wanawake wenzake kijijini hapo, ndipo akaanza kujifunza unahodha kwa sababu ya kunyanyasika wakati wakihitaji usafiri wa mashua baharini kwa ajili ya shughuli hiyo ya uvuvi wa chaza.
“Baadhi ya manahodha wanaume wakitukejeli kwa maneno ya kutuvunja moyo, wakati tunahitaji usafiri wakituambia kuwa katika chombo hatupakii wanawake.
“Kama mnaweza kuendesha chukuweni chombo muendele, tukakaa kwa Pamoja, tukasema madhila haya yatatukumba mpaka? Hebu tujitokezeni tujifunze sisi wanawake kuendesha,” anasimulia chimbuko lake.
Hapo anasimulia wakajitokeza baadhi ya wanaume kuwafundisha na yeye akawa pekee aliyejitokeza kujifunza, leo hii sasa kawa mjuzi wa uendeshaji chombo cha usafiri baharini jasiri na asiye na woga majini.
Nahodha huyo mwanamke anasema kabla ya kujikita kusafirisha watalii, akawa anawasafirisha wanawake wenzake wavuvi wa chaza, kutoka sehemu moja kwenda kwingine baharini, kwa ajili ya uvuvi huo.
“Tangu nianze kuendesha chombo hiki cha baharini inafika miaka 20, lakini kwa kusafirisha watalii visiwani kwa sasa nina muda wa miaka mitano” anasimulia Nahodha Bahati.
SURA YA CHANGHAMOTO
Kuhusu changamoto ya kazi yake, anataja kuwapo wakati mwingine mashine ya mashua huharibika wakiwa safarini katikati baharini na wageni huwa hawaamini kufkishwa salama, pia changamoto ya ‘Upepo wa Kusi na Kaskazi…” anasema
Nahodha huyo anasema, matarajio yake baadaye ni kumiliki mashua yake, kwani anayofanyia kazi sasa sasa ni ya kukodi, hivyo kipato cha hukigawanya na mmiliki.
Hata hivyo, yu katika hatia amekuwa gumzo kwa baadhi ya wanawake kijijini anakotoka, wakimuelezea kuwa mwanamke jasiri na asiyeogopa madhila ya baharini, hasa wakimhsudu anavyoendesha boti hilo kwa ufanisi, akisafirisha wageni wake watalii.
“Sisi ni wanawake, lakini hatuna ujasiri kama wake wa kuingia majini na kuendesha chombo cha bahari kama yeye. Lakini, tunamhusudu na tunamuombea kwa Mungu ampe nguvu na kumuongezea ujasiri.
“Maana angekuwa na hofu kama sisi wengine, asingeweza ‘kuteremesha’ chombo na angetetemeka akashindwa njiani. Lakini, tunamsifu sana yeye ni Hodari!” anatamka mwanamke anayejitambulisha jirani yake wa karibu, pasipo kufafanua jina lake.
Sheha (Katibu Kata) wa Shehia ya Kikungwi, Muhammed Haji Ushahidi, anamtaja Bahati mwanamke wa mfano katika kijiji hicho, hata kimaendeleo anawasaidia kujikwamua kiuchumi.
“Bi Bahati ni jasiri! Ni mwanamke anayejiamini, mwanamke anaepambana kutafuta maisha, ni mwanamke anayejielewa, kwa sababu ‘wanawake ‘wanaweza wakiwezeshwa’, lakini wapo wanawake ambao wanaogopa kujitoa, niwaombe wajifunze kwa Bi Bahati jinsi anavyojitoa,” anasema.
Sheha huyo, anamsifu kwamba ni wa kujitoa na nguzo kubwa kijijini kwake, maana licha ya kuendesha boti, pia ana kazi ya kuhudumia watalii visiwani, akionekana anafaa kwa ufanisi.
Anawafafanua, wanawake kijijini aliko wamegawanyika kwenye makundi, katika nyendo zao za kutafuta kipato, wapo waliojikita katika uvuvi wa samaki chaza.
ALIYEMFUNZA UNAHODHA
Khamis Juma Mwalimu ni mwalimu wa Bahati kuendesha boti, anasema mwanafunzi wake huyo sasa ni mvuto wa wageni, wengi wapofika hapo hupendelea kusafirishwa na Bahati.
“Huyu Mama ni mwanafunzi wangu, kwa kweli ni mwanamke hodari, anayejituma na wala haoni aibu katika kufanya kazi yoyote ya kujipatia kipato,” anasema.
Ni hoja inayopokewa na Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam, Dk. Tumaini Gurumo, anayesema ushiriki wa wanawake katika masuala ya bahari sio mkubwa, wengi wamejikita katika usajili wa usafirishaji wa meli.
Dk. Gurumo anaeleza kwamba, katika nafasi ya ubaharia, bado idadi ni ndogo na kuna kazi kubwa ya kuwashawishi wakijikite katika nafasi hiyo.
Hata hivyo, anawatoa hofi kwamba, nafasi ya ajira baharini hazitazami jinsia, kwani hata sheria za kimataifa zimebadilika, zikimpa nafasi mwanamke kuingia baharini na kupata haki anazostahili, sawa na mwanaume.
Anataja mzizi wa kasoro ulioko sasa inatofautiana na zamani, kuwa ‘mtoto wa kike hawezi kufanya kazi za baharini’. Anasisitiza, mtazamo huo wa kale uliwazibia fursa na lazima wanawake sasa wapewe nafasi kujikwamua, familia zao na taifa kwa ujumla.
Kisiwa cha Zanzibar kina ajira nyingi za baharini, hivyo ili nchi kuendelea kutoweka mipaka baina ya wasichana na wavulana lazima wote kuwapa nafasi kuingia katika fani hizo na kusaidia nchi na jamii.
“Wapo wasichana tuliowafundisha sasa ni manahodha na wahandisi kwenye Meli kwa hivyo sio neo la kusema ni tambuu kama zamani hivi sasa milango ipo wazi, teknolojia imekuwa hakuna meli itakayozunguka kukaa baharini kwa muda mrefu kutoka bandari moja kwenda nyengine, hivyo ipo nafasi kwa wasichana”alisema Dk Gurumo.