Hayo ni maoni ya baadhi ya wadau wa elimu baada ya ripoti ya upimaji viwango vyuo vikuu Kusini mwa Jangwa la Sahara, kuonyesha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambacho ni kikongwe nchini, kuporomoka hadi nafasi ya 21 kutoka kwenye 10 bora.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, vyuo 10 bora katika ukanda huo na nchi kwenye mabano ni vinne (Afrika Kusini), viwili (Tanzania) huku nchi za Uganda, Rwanda, Nigeria na Ghana vikiwa na chuo kimoja kila moja.
Wakati UDSM ikionekana kuporomoka kwa ubora, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) vimevyoingia kwenye vyuo vikuu 10 bora.
Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti, baadhi ya wasomi wamechambua chanzo cha kuporomoka viwango na ubora wa vyuo nchini.
Dk. Peter Kafumu, mwalimu wa chuo na mtumishi wa umma, alisema ukosefu wa maprofesa ni sababu kubwa inayoporomosha ubora wa elimu ya vyuo nchini. Alisema vyuo vikuu vingi vya umma na binafsi havina wanataaluma (wahadhiri na maprofesa) kutokana na sababu mbalimbali.
Alisema vyuo hivyo vinakosa maprofesa wabobezi na hakuna programu ya kuwaandaa warithi wa taaluma zao ili kuchukua nafasi baada ya kustaafu au kuondoka.
“Nimesoma chuo kikuu Ubelgiiji, nilishuhudia profesa mmoja awe wa jiolojia au kemia ana wasaidizi wawili ambao ni wahadhiri ili anapoondoka awe ameshiriki kuwaandaa warithi ambao pia wanapanda ngazi na kuziba nafasi yake,” alisema.
Akirejea hali ya vyuo, alisema maprofesa wengi wamestaafu na hakuna wengine wa kuwarithi na kwamba ndicho chanzo cha kuporomoka kwa ubora.
Dk. Kafumu alisema ufumbuzi wa tatizo hilo ni kuwa na programu ya kuandaa na kurithisha ujuzi na utaalamu wenye utaalaamu, viwango na ujuzi watakaochukua nafasi za wabobezi wanapostaafu.
Mhadhiri mstaafu wa MUHAS, Dk. Eva Marie Semakafu, alisema tatizo ni utaratibu wa kuandaa wahadhiri wa vyuo vikuu kwa kuangalia ufaulu wa juu (GPA) kwa kumpa ajira aliyepasi sana badala ya kuangalia ubobevu na umahiri wa mwanafunzi tangu anapojiunga na chuo kwenye somo analotakiwa kulifundisha.
Alisema inawezekana mwanachuo akafaulu kwa alama A zote lakini hana sifa za kuwa mhadhiri wala kufundisha chuo si ndoto yake.
Dk. Semakafu alisema kuna haja ya kuangalia taratibu za kuandaa wanataaluma katika vyuo kwa vigezo vinavyotumika siku zote badala ya kutegemea GPA kubwa.
Pia alisema serikali kusitisha ajira za wanataaluma vyuo vikuu kwa muda mrefu limesababisha ombwe kwenye ngazi mbalimbali kuanzia wanaochipukia, waandamizi hadi wabobezi. Hali hiyo, alisema imesababisha upungufu mkubwa wa maprofesa hasa pale ambapo profesa anapostaafu kwa vile anakosa mrithi.
Mwanataaluma huyo mstaafu alisema wingi wa wanafunzi vyuoni hauendani na uwiano wa wanataaluma huku pia akibainisha kuwa miundombinu pia haitoshi katika vyuo vikuu vya umma na binafsi.
Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA, Dk. Donald Mmari, alisema japo hafahamu vigezo wanavyotumia kupima ubora wa vyuo vikuu, aligusia wingi wa wanavyuo kuwa ni mzigo kwa ufanisi.
“Mambo ya kuangalia ni pamoja na kudahili wanafunzi wengi wakati hakuna miundombinu, wahadhiri, maprofesa, mafunzo kwa vitendo, teknolojia ya kisasa na maktaba kuwezesha kupata elimu yenye ubora,” alisema.
Alisema ufumbuzi wa tatizo hilo ni kufikiria na kutekeleza sera mpya ya elimu inayotaka wanafunzi kupata ujuzi na elimu ya ufundi katika vyuo vya kati vya awali badala ya wote kwenda vyuo vikuu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Dk. Kaanaeli Kaale, alikumbusha kuwa viwango hivyo hupimwa kwa kutazama idadi na ubora wa machapisho ya wahadhiri na maprofesa wa vyuo vikuu ambayo huandikwa kwenye majarida ya kimataifa na kuangaliwa jinsi yanavyoongeza thamani na ubora kwenye elimu.
Alisema ukosefu wa wahadhiri na maprofesa umetokana na vyuo vingi vya umma kutokuajiri kwa kuwa serikali ilisitisha ajira zao na kuongeza ombwe linaloshusha ubora wa elimu ya juu.
Nafasi ya kwanza na ya pili inashikiliwa na Witwatersrand, Johannesburg mtawalia (Afrika Kusini), MUHAS, Pretoria (Afrika Kusini), Makerere (Uganda), Western Cape (Afrika Kusini), Covenant (Nigeria), UGHE (Rwanda), Ashesi (Ghana) na Ardhi (Tanzania).










