Kikwete: Membe alikuwa msaada mkubwa kwangu kikazi na kisiasa

14May 2023
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Kikwete: Membe alikuwa msaada mkubwa kwangu kikazi na kisiasa

RAIS mstaafu wa awamu ya nne, Dk. Jakaya Kikwete, amefunguka kuhusu aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bernard Membe, kwamba alikuwa mtu wa msaada mkubwa kwake katika maisha ya kikazi na kisiasa.

Kikwete amesema wametoka mbali na Membe, alitumika katika wadhifa huo kwa miaka minane wakati wa serikali yake, wamesaidiana kwa mengi.

Membe alifariki dunia juzi asubuhi katika Hospitali ya Hurbert Kairuki, Mikocheni mkoani Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuzidiwa ghafla.

Viongozi mbalimbali wa serikali, taasisi, vyama vya siasa jana waliendelea kumiminika nyumbani kwa marehemu Membe Mikocheni kwa ajili ya kuhani msiba huo.

Katika salamu zake za rambirambi alizozitoa juzi kwa mke wa Membe, Mama Dorcas Membe, Kikwete amefunguka mambo mbalimbali.

Katika taarifa yake, Kikwete alisema, “Familia zetu na mapito ya maisha yetu yamehusiana sana.”

Alisema Membe alikuwa mtu wa msaada mkubwa kwake katika maisha yake ya kikazi na kisiasa.

“Nilimwamini na kumtumainia katika nafasi zote alizohudumu kwenye baraza langu la mawaziri.

“Aliwahi kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Nishati na Madini. Hali kadhalika, aliwahi kuwa Waziri wangu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa miaka tisa ambapo alifanya kazi kubwa na nzuri ya kuendeleza maslahi ya Tanzania katika medali za kimataifa,” aliandika Kikwete na kuongeza:

“Ninautambua mchango wake mkubwa aliotoa kwenye Chama Cha Mapinduzi alipokuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Mjumbe wa Kamati kuu na Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa katika Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa. Katika nafasi zote hizo, alijitoa kwa moyo wake wote na kuacha alama za kudumu,” alisema.

Pia alisema anamfahamu Membe kama mwanadiplomasia mbobezi, mwanamikakati makini, msomi mzuri, mcha Mungu, mzalendo, mchapakazi hodari na mtu jasiri ambaye hakuogopa kusema na kulisimamia analoliamini.

“Hakika taifa limepoteza mmoja wa watu muhimu. Ninatoa salaam za rambirambi na mkono wa pole kwako shemeji yangu, Dorcas Membe na watoto wetu, Cecilia, Richard na Dennis pamoja na wajukuu, ndugu na jamaa wa marehemu Membe. Nawapeni pole kwa msiba mkubwa uliowakuta.

“Lakini, ninapenda kuwahakikishia kuwa hamko wapweke. Mimi pamoja na mke wangu Salma na wana familia wetu wote, tuko pamoja nanyi katika majonzi na kuomboleza. Tunawaombea kwa Mola awajalie moyo wa subira na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu mnachopitia,” alisema.

Kikwete akamalizia kwak usema: “Tukumbuke daima sisi sote ni waja wake, na kwake tutarejea’. Bwana ametoa Bwana ametwaa, Jina lake lihimidiwe. Tumwombee kwa Mola marehemu mpendwa wetu, apumzike kwa amani na roho yake aiweke mahala pema peponi. Amina.”

Katika Wizara Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (sasa Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki), Membe alihudumu kama Waziri kwa miaka tisa hadi 2015, akiwa mtu wa pili kushika wadhifa huo kwa miaka mingi, akitanguliwa na Kikwete aliyeshika kwa miaka 10.

MPANGO ATOA POLE

Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, kupitia ukurasa wake wa Instagram aliandika: “Ninaungana na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan, kutoa pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na watanzania kwa ujumla kufuatia kifo cha aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, marehemu Bernard Membe.

“Mwenyezi Mungu akawe mfariji wa familia na wote walioguswa na msiba huu. Ninamuombea marehemu apumzike kwa amani.”

Akizungumza nyumbani kwa marehemu, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, alisema tofauti zao za kiitikadi hazikuutofautisha ukaribu wake na kwamba yalikuwapo mambo waliyoshirikiana.

Alisema licha ya kero alizowahi kufanyiwa na serikali ya CCM haiondoi ukweli kuwa bado wana uhusiano na baadhi ya viongozi wake.

Kiongozi huyo wa CHADEMA alisema Membe alikuwa mtu asiyekasirika na hata ikitokea hivyo alionyesha tabasamu.