Kichanga kilichoibwa Geita chapatikana hai Chato

06Jan 2024
Daniel Limbe
Chato
Nipashe
Kichanga kilichoibwa Geita chapatikana hai Chato

WIKI mbili baada ya Martha Phelemon, Mkazi wa Ludete Jimbo Busanda mkoani Geita, kuripoti kuibiwa mtoto wake mchanga baada ya mama huyo kwenda bafuni kuoga, hatimaye mtoto huyo amepatika akiwa hai wilayani Chato mkoani humo huku mtuhumiwa akiendelea kuhojiwa kabla ya kufikishwa mahakamani.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita,ACP Amon Mimata, amesema kuwa jeshi hilo limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa,Swaumu Mahondola (32) ambaye ni Mkazi wa Kijiji cha Kibumba Kata ya Makurugusi wilayani Chato baada ya uchunguzi wa kina kupitia mtandao wa simu na kwamba mtoto huyo tayari amerejeshwa kwa wazazi wake baada ya uchunguzi wa kitabibu kuthibitisha kuwa ni buheri wa afya.

Amesema taarifa za kuibiwa mtoto huyo mwenye mwezi mmoja ziliripotiwa Desemba 22, 2023 kwenye kituo kidogo cha Polisi Katoro na uchunguzi wa haraka ulianza ikiwa ni pamoja na kupata namba za simu za mshukiwa wa uharifu huo kabla ya kufanikiwa kumnasa akiwa na kichanga hicho.

Aidha ACP. Mimata, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi mkoani humo ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa haraka za matukio ya kiharifu kabla na baada ya kutokea ili yaweze kudhibitiwa haraka kabla ya kusababisha madhara kwa Umma.