Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa tatizo hilo linazidi kushika kasi kulinganisha na miaka ya nyuma na kwamba baadhi ya magonjwa hayo yalikuwa yakiwapata watu wazima. Hali hiyo imeilazimu Nipashe kupiga hodi kwa madaktari bingwa ili kufahamu nini kisababishi kikuu.
Mtaalamu wa magonjwa ya watoto katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Mbeya, Dk. Boniface Mariki, amesema ziko sababu mbalimbali zinazofanya watoto kuzaliwa wakiwa na magonjwa yasiyoambukiza.
Dk. Mariki alisema baadhi ya magonjwa ambayo watoto wanazaliwa nayo ni pamoja na kisukari, mgongo wazi pamoja moyo.
Alisema moja ya sababu ni pamoja na kinamama kutohudhuria kliniki wakati wa ujauzito, hivyo kukosa elimu pamoja na baadhi ya dawa muhimu ambazo wanatakiwa kuzitumia.
Baadhi ya watoto, alisema wanazaliwa na kisukari kutokana na kurithi ugonjwa huo kutoka kwa mama au kupata maambukizi ambayo yanashambulia kongosho, hivyo kushindwa kuchuja sukari.
“Watoto kuzaliwa na matatizo ya mgongo wazi na kichwa kikubwa husababishwa na kinamama kutofuata masharti wanayopewa na wataalamu hospitalini wakati wa ujauzito hasa kumeza vidonge vya kuongeza damu na madini ya folic acid,” alisema Dk. Mariki.
UVUTAJI SIGARA
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake, Dk. Cosmas Kapinga, anabainisha kwamba sababu zinazosababisha mtoto kuzaliwa na magonjwa yasiyoambukiza ziko nyingi kama vile kurithi, ukosefu wa lishe kwa mama mjamzito au mtoto.
Alisema sababu nyingine ni jamzito kuvuta sigara wakati wa miezi mitatu ya ujauzito hali inayoweza kusababisha mtoto kuzaliwa na tatizo la moyo, presha au kisukari.
“Hata matumizi ya pombe kwa mama mjamzito, matumizi ya dawa za kulevya, matumizi ya dawa za malaria, minyoo kipindi cha miezi mitatu ya ujauzito yanaweza kusababisha mtoto kuzaliwa na magonjwa yasiyoambukiza,” alisema Dk. Kapinga.
Dk. Kapinga alisema sababu nyingine ni majeraha kwa mjamzito wakati wa kujifungua, kwamba anaweza kumbana mtoto kichwa na kusababisha mtoto huyo kuzaliwa akiwa taahira.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake kutoka Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH), Dk.Harry Mwambe, anaeleza kuwa kinamama kuwa na tatizo la sukari ni moja ya sababu ya kuzaa watoto wenye ugonjwa huo.
“Shida kubwa ni kinamama wengi hivi sasa kuwa na shida ya sukari nyingi, hivyo mtoto anapozaliwa ana ‘adopt’ hali ile ndiyo maana unakuta hivi sasa kumekuwa na tatizo la idadi kuwa ya watoto wadogo kuwa na shida ya ugonjwa wa sukari,” alisema.
Alibainisha kuwa mtindo wa maisha nao umekuwa chanzo kikubwa cha kuongezeka kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
“Hivi sasa watu wanakula hovyo vyakula unakuta mtu ana uzito mkubwa kuliko urefu wake, hivyo inatakiwa watu kuanza kula vyakula salama lakini pia kufanya mazoezi ili kuondokana na tatizo hili la magonjwa yasiyo ya kuambukiza,” alisema Dk. Mwambe.
Dk. Salha Nassoro Rashid kutoka Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Manyara alisema miongoni mwa magonjwa ambayo watoto wanazaliwa nayo ni vichwa kujaa maji, utumbo kuwa nje na kuzaliwa bila kuwa na sehemu ya haja kubwa.
Alisema tatizo la watoto kuzaliwa na vichwa maji maarufu vichwa vikubwa lipo kwa wingi huku akibainisha kuwa idadi yao si kubwa sana kwa mwezi, kwamba wanapokea mtoto mmoja na wengi wao wanakuwa wamepewa rufani.
Pia alisema kuhusu utumbo kuzaliwa ukiwa nje ni tatizo ambalo lipo na kwa wiki wanapokea watoto wawili.
Daktari kutoka Idara ya Upasuaji wa Ubongo na Mfumo wa Fahamu Hospitali ya Rufani ya Kanda Bugando, David Kambale, alisema uzembe, ulaji wa vyakula, mtindo wa maisha ni chanzo cha magonjwa hatari kwa watoto.
Alisema ongezeko la watoto wanaozaliwa na matatizo mbalimbali ikiwemo magonjwa ya saratani, vichwa vikubwa pamoja na mgongo wazi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa vimekuwa vikisababishwa na tatizo la kinamama kutokujali mienendo ya maisha kila siku.
Alisema zaidi ya watoto 1,000 kutoka mikoa mbalimbali ya ndani na nje ya Kanda ya Ziwa hupokelewa katika Hospitali ya Rufani ya Kanda Bugando wakiwa na magonjwa ya saratani, vichwa vikubwa na mgongo wazi. Alisema hizo ni takwimu kuanzia Oktoba, 2021 hadi Oktoba, mwaka jana.
Alisema ugonjwa wa kichwa kikubwa kitaalamu hujulikana kwa jina la ‘Hydrocephalus’ ikiwa jina hilo linatokana na neno la Kigiriki lenye maana ya maji ndani ya kichwa, alieleza kuwa si kila mwenye kichwa kikubwa ana ‘hydrocephalus’.Dk. Kambale alieleza watoto 700 hupokewa kwa mwaka katika hospitali hiyo ili kufanyiwa upasuaji, akisema tatizo hilo linatokana na ubongo kuwa na kiasi fulani cha majimaji.
Kuhusu tatizo la mgongo wazi, Dk. Kambale alisema ugonjwa huo kwa jina la kitaalam huitwa ‘spina bifida’, ambapo ni ugonjwa au hali ambayo mtoto anazaliwa nayo huku uti wa mgongo ukiwa wazi, kutokana na mifupa kutokufunga vizuri.
Alisema kwa kawaida baada ya mimba kutunga uti wa mgongo hutengewa nusu upande mwingine na nusu upande mwingine na baadae kuungana, kwamba wakati wa muunganiko huo ndiyo kasoro inaweza kutokea na hivyo sehumu fulani ikawa haijaziba vizuri na kuacha tundu.
Alisema tatizo hilo linaweza kusababishwa na mjamzito kufanyiwa kipimo cha mionzi (X-ray), matumizi ya dawa za kifafa, upungufu wa ‘folic acid’ yaani dawa za vitamin B9 zitolewazo katika zahanati wakati wa klimiki.
Pia alisema ugonjwa huo unaweza kumpata mtoto yeyote ambaye mama yake hakupata virutubisho kabla ya kushika mimba ikiwa kwa kawaida virutubisho hivyo hupatikana katika vyakula vyenye protini na vina uwezo wa kumzuia mama kwa asilimia kubwa asipate changamoto ya kuzaa mtoto mwenye ulemavu huo.
Daktari wa magonjwa ya saratani kwa watoto kutoka hospitalini hiyo, Dk. Heronima Joas, alisema ugonjwa wa saratani kwa watoto nao ni tishio nyakati hizi, huku sababu kubwa zikidaiwa kuwa pamoja na wajawazito kutumia samaki wanaovuliwa kwa kutumia kemikali aina ya zebaki zinazohusishwa na maambukizi ya saratani kwa mtoto kipindi akiwa tumboni.
Alisema mpaka sasa wataalamu bado hawajabaini sababu hali za magonjwa ya saratani kwa watoto, lakini kunavitu baadhi ambavyo vinahusishwa na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na uvuvi wa kemikali.
Imeandaliwa na Jaliwason Jasson (BABATI), Paul Mabeja, (DODOMA), Vitusi Audax (MWANZA) na Nebart Msokwa (MBEYA)










