Filamu hiyo iliyotafsiriwa kwa lugha ya Kifaransa, itaonyeshwa katika mabasi ya kampuni hiyo yanayosafirisha abiria katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kiongozi huyo alitoa pongezi hizo, kwenye hafla ya uzinduzi wa uonyeshaji wa filamu hiyo kwenye mabasi hayo iliyofanyika kwenye viwanja vya ubalozi wa Tanzania nchini DRC, Kinshasa jana na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwamo maofisa wa Ubalozi wa Tanzania na wawakilishi wa kampuni hiyo.
Pia alimpongeza Balozi wa Tanzania DRC, Said Mshana, na timu yake kwa kufanikisha jambo hilo alilosema ni la muhimu na la kuungwa mkono.
Dk. Tax alisema balozi huyo ana mwaka mmoja tangu alipoteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo lakini katika kipindi hicho kifupi amefanikisha mambo mengi makubwa na muhimu.
“Amefanya mambo makubwa likiwamo hili la kuishawishi kampuni ya Classic yenye mabasi 50 inayotoa huduma ya usafiri wa abiria katika miji mbalimbali ya Congo, ikiwamo ya Kinshasa na Lubumbashi, kutangaza filamu ya the Royal Tour bila malipo,” alisema.
Alisema mabasi ya kampuni hiyo inayomilikiwa na Mtanzania Amir Abdallah, anayeishi nchini humo hayatumiwi na Wacongo pekee, bali na raia wa nchi zingine, hivyo ni fursa katika kutangaza Tanzania na uwekezaji, biashara pamoja na utalii ili kutimiza azma ya serikali ya kuvutia watalii milioni tano na mapato ya Dola za Kimarekani bilioni sita ifikapo mwaka 2025.
Pia alitoa wito kwa kampuni zingine na sekta binafsi kwa ujumla kujitokeza kushirikiana na Serikali katika jitihada za kukuza uchumi ikiwa ni pamoja na kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazopatikana Tanzania.
Waziri huyo kwenye hotuba yake, alisema hafla hiyo ni sehemu ya kusherehekea miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Tanzania Machi 19, 2021 na mafanikio mengi yamepatikana katika kipindi hicho cha uongozi wake.










