Amesema sheria ni mizani hivyo aliyeshindwa pia anaweza akapata haki yake kwa kukata rufaa.
Ameyasema hayo jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha siku tatu cha majaji wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
“Siku hizi tumezoea kuona baadhi ya watu wanatoka mahakamani wanatafuta kamera na video (waandishi wa habari) na kuanza kusema haki imepotea bila kuangalia mizani iliyokuwa mahakamani, ninawaomba (majaji) msikatishwe tamaa na wale wanaotoka mahakamani na kusema mahakamani hakuna haki wakati wameacha mizani mahakamani,” amesema.
Prof. Juma amewaomba wadau wa Mahakama waendelee kuwaelimisha wananchi kuwa haki siyo ushindi, bali haki ni ushahidi uliotolewa mahakamani, sheria iliyotumika kwenye kutoa uamuzi na mizani ambayo imetoa haki hiyo.
Aidha amesema haki ni eneo pana japo kwa siku za karibuni wanaona baadhi ya wananchi wanapotoka mahakamani wameshindwa kesi huangalia haki kwa upande mmoja tu.
Pia amesema ushirikiano na wadau ni lazima na viongozi wawasikilize wananchi na kutumia changamoto zao kufanya maboresho na mabadiliko.
Jaji Kiongozi Mustapher Siyani, amesema idadi ya kesi za mlundikano katika mahakama hizo umepungua kutoka mashauri 878 mpaka 455 katika mahakama za hakimu mkazi na kutoka mahakama za wilaya na za mwanzo kutoka 19 hadi sifuri.
Amesema tangu kufanyika kikao kazi kama hicho mwaka 2022 muda wa wastani unaotumika tangu shauri kufunguliwa mpaka kumalizika umepungua kutoka siku 321 hadi 262.
Kadhalika amesema mlundikano wa idadi ya mashauri umepungua kutoka asilimia tano hadi mbili.









