Jaji Mkuu akerwa na mawakili kutumia lugha zisizo na maadili

03Dec 2023
Kulwa Mzee
Nipashe Jumapili
Jaji Mkuu akerwa na mawakili kutumia lugha zisizo na maadili

JAJI Mkuu, Prof. Ibrahim Juma, amesema amepokea malalamiko kutoka kwa majaji kuhusu mawakili wa kujitegemea kutumia lugha zinazokiuka maadili ndani ya mahakama.

JAJI Mkuu, Prof. Ibrahim Juma.

Kutokana na hali hiyo, amekitaka Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kuchukua hatua kabla ya majaji kulalamika.

Prof. Juma alibainisha hayo katika hafla ya kuwakubali na kuwatunuku vyeti mawakili wapya 279. Kati ya mawakili hao wapya, wanawake ni 118 na wanaume 161.

Alisema nasaha zake kwa mawakili hao anazielekeza katika maeneo matano, ambayo ni maadili, wajibu wao kwa mahakama na jamii, nani wanafaa kuwaiga kufanya kazi, uwezo na tahadhari.

“Kila mwaka tunazungumzia maadili, asilimia 99 ya kazi za uwakili zinategemea maadili. Tukiififisha  mahakama tunafifisha taaluma. Ukikubaliwa kuwa wakili unachukuliwa kuwa una uwezo.

“Uwezo ukitoweka unaingia katika hatua ya kuvunja maadili, tuwe waangalifu katika eneo la maadili, kwani linachafua taswira yote ya sheria,” alisema Jaji Mkuu.

Alisema uwakili ni taaluma yenye heshima, vitendo, kauli, saini na mihuri vyote vinatakiwa kuwa na heshima.

“Kila taaluma duniani inategemewa itajidhibiti na kuwadhibiti wanachama wake. TLS ikifanya hivyo hakuna mtu wa kuwaingilia, tofauti sasa chombo kikichukua hatua mawakili wanakusanyika kutetea.

“Sasa chama chenyewe kichukue hatua za kinidhamu, tumieni mamlaka mliyonayo kujidhibiti wenyewe, tumieni kanuni zenu za uwakili za mwaka 2022 kujidhibiti ni wajibu kuonyesha nidhamu kwa mahakama,” alisisitiza.

Prof. Juma alisema amepokea malalamiko kadhaa kutoka kwa majaji kuhusu lugha zinazotumika mahakamani na mawakili na kwamba majaji wanatumia busara kwa kuwa zinakiuka Kanuni ya 92 ya Maadili ya Mawakili.

"Wakili ukijibizana na majaji au hakimu unakiuka kanuni zenu. Ikitokea tukio kama hilo isiwe hadi jaji alalamike, mawakili wachukue hatua likitokea kwa kumchukua wakili husika na kumfikisha kwenye vyombo na kutoa adhabu, "alisema Jaji Mkuu.

Kabla ya kuzungumza hayo aliwakubali na kuwatunuku vyeti mawakili hao 279.

"Kwa mamlaka niliyopewa na Sheria ya mawakili sura ya 341 Toleo la 2019, kifungu cha 8(3) nina tamka kwamba wale wote ambao majina yao yamesomwa hapa wamekubaliwa kuwa mawakili na wameorodheshwa rasmi kwenye orodha ya mawakili kuanzia leo Desemba Mosi,” alitamka Jaji Mkuu.

Alisema idadi hiyo ya mawakili wapya inafanya jumla ya mawakili sasa kufika 11,916 kutoka idadi ya awali ya mawakili 11,636.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais wa TLS, Harold Sungusia, alisema wako katika operesheni ya kupambana na mawakili vishoka katika maeneo yote.

Sungusia alisema wanajitahidi kusimamia vyema maadili, mihuri holela na wanahakikisha mihuri ya mawakili haighushiwi.

Alisema wameanzisha kituo suluhishi cha migogoro ya ndani na nje ya nchi ili kupunguza msongamano wa kesi mahakamani.

Sungusia aliwataka mawakili wapya kusimamia haki za wateja bila kupendelea wala kuogopa.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Eliezer Feleshi, akizungumzia vishoka, alisema ikithibitika adhabu yake huwa ni faini ya Sh. milioni tano hadi Sh. milioni 20 au kifungo mwaka mmoja hadi miaka isiyozidi mitatu au adhabu zote kwa pamoja.

“Ninawaonya wanaofanya udanganyifu huo kuacha mara moja kutochukua hatua kunadhoofisha taaluma. Hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya mawakili wa kujitegemea wanaokiuka maadili wakiwamo vishoka,” aliagiza Dk. Feleshi.