Hiki ndicho kiini cha vijana kutowajibika katika ndoa

26Mar 2023
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Hiki ndicho kiini cha vijana kutowajibika katika ndoa

KASI ya vijana hasa wa kiume kutowajibika katika nafasi zao kwenye ndoa imekuwa ikiongezeka kila uchao.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Dk. Charles Kitima,

Hatua hiyo imewaibua viongozi wa kidini, kimila na wazazi ambao wamebainisha mambo kadhaa wanayoamini ndicho kiini cha mmomonyoko wa maadili  kwa vijana wa kiume,  unaochangia kushindwa kwenye nafasi zao katika ndoa.

Baadhi ya mambo yanayotajwa ni pamoja na malezi, mila kusahaulika, kujilea au kulelewa na watu wasio na maadili na wazazi kutumia muda mwingi katika kazi badala  ya malezi ya watoto.

Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwapo kwa janga hilo, vijana wengi wanajiingiza kwenye mapenzi na wanawake umri mkubwa ili kulelewa na wengine kukimbia ndoa.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Dk. Charles Kitima, alisema katika makuzi ya mtoto kwenye familia, wazazi wanapaswa kuwa mfano wa kuwawajibisha na kuwafundisha kazi ili wajue kuishi kwa kujitegemea.

“Lakini pia akiwa shuleni, kuanzia shule za msingi zinasisitiza maadili ya kuwajibika na kujua mipaka ya maisha na uhuru. Tukumbuke kufundisha na kutenda inategemea mzazi atafuatilia vipi matendo ya mtoto wake tangu mdogo kuona kama yanaendana na anavyolelewa shuleni.

“Ni wazi kuwa, kwa sasa changamoto kubwa ni hii, wazazi wanakaa na watoto muda gani? Wana muda wa kutosha wa kupima tabia zao? Jibu ni hapana,” alisema.

Dk. Kitima alisema usimamizi wa tabia unapaswa kuangaliwa shuleni lakini utengenezaji tabia huko nyuma ulifuatiliwa zaidi na mzazi.

“Watoto walikuwa wanakwenda kufanya shughuli pamoja na wazazi wao kabla haya mambo ya wazazi ya kutokuwa na muda nao kwamba wako ‘busy’ hayajaanza. Hata shuleni kulikuwa na vipindi vya watoto wanafanya kazi na wanafuatiliwa, wanapewa adhabu wanalima.

“Ukienda nchi nyingine unakuta watoto wamewekwa kwenye makundi mbalimbali kujifunza tabia ya kuwajibika, haya yote ni kuwafanya wajifunze tabia ya uwajibikaji, kujitolea na kujituma na kuonyesha uwezo wa kujitegemea. Hivi sasa mtoto hawajibishwi kuchota maji, kufua hata kulima bustani, haya yote yanasababisha baadaye ashindwe kufanya kazi ya aina yoyote,” alisema.

Tatizo lingine analitaja kuwa ni kwa watoto wanaosoma shule za mjini, kazi si sehemu ya malezi hivyo, na wenyewe wanafikiri kwamba atakuja na kukuta fedha na ndizo zitafanya kazi na si yeye.

Padre Kitima aliwakumbusha wazazi kuwa malezi ya mtoto ni lazima ajengewe hofu ya Mungu ili wajue neno Mungu si la kutamka tu bali linapaswa kuishi. Pia alisema ni lazima wahakikishe wanafunda tabia za watoto wao ili wengine wamwone ana vigezo vya kijamii na kukubalika kila hatua ya maisha ya mtoto.

“Mtoto anapojitegemea wazazi huwatenga, mila na dini hutengwa ndiyo maana unakuta vijana wengi wanashindwa kuanzisha familia na wanaoanzisha wanakimbia,” alisema.

KUVUNJIKA NDOA

Alisema kuvunjika kwa ndoa nyingi kunasababishwa na kutofuata taratibu za kimila za kuanzishwa familia na maandalizi ya malezi yanayoanza utotoni ikiwamo jando ambalo hutumika kuwaandaa kuwa wanaume thabiti wanaoweza kuwajibika kutunza ukoo na kabila.

Chifu Mkuu wa Wasafa kutoka Mbeya, Loketi Mwashinga, alisema kwa sasa limekuwa jambo la kawaida kumkuta kijana mwenye umri mdogo, akilelewa na mwanamke mtu mzima na akiwa hana wasiwasi wowote.

Alisema wanafanya hivyo kwa sababu hawataki kujishughulisha zaidi ya kutafuta urahisi wa maisha kwa wanawake waliowazidi umri au wenye umri wao ambao wana uwezo wa kipato.

Chifu Mwashinga alisema vijana wa sasa wamekuwa tofauti na mila zilizowalea wazazi wao na kilichowafikisha kuwa hivyo ni utandawazi.

“Ili kuwarudisha kwenye mstari ni lazima serikali ikubali kushirikiana na wazee wa mila kila mkoa ambao wao watasaidia kuelimisha na kukemea vitendo vinavyofanywa na vijana tofauti na mila na desturi, wakati mwingine unaweza kuogopa kukemea maana wana lugha chafu na wanaweza kukupiga.

“Maadili ya watoto yanaanzia kufundishwa nyumbani, walimu wanapokea pamoja na jamii. Kuna tukio hapa Mbeya lilitokea shule moja ya sekondari ilikuwa inaongoza kwa matukio ya mimba. Tuliposhirikishwa tulitoa kauli moja kwamba mtoto atakayempa mimba binti, tutamhamishia ailee wakati binti akiendelea na masomo, mpaka sasa hakuna mimba tena” alisema.

Mwenyekiti wa Kamati za Amani na Jumuiya ya Maridhiano Tanzania, Shekhe Alhad Mussa Salim, aliwakumbusha wanaume kwamba jukumu walilobeba ni la kumsimamia mwanamke ikiwa ni pamoja na kutimiza wajibu  wa kumlisha, kumvisha na kumpatia makazi.

“Mwanamke akifanya majukumu hayo huwa ni hisani si wajibu wake na anapofanya hivyo hupata dhawabu, kitendo cha mwanaume kuanza wajibu wake anapoteza heshima yake”, alisema huku akitoa wito kwa vijana kwamba wasikwepe majukumu yao na kutafuta kulelewa.

Jumanne Hassan, mkazi wa Mwenge mkoani Dar es Salaam, alisema kitendo cha baadhi ya vijana wa kiume kutowajibika kwenye majukumu ya familia au kujishughulisha kinasababishwa na kupenda maisha rahisi.

“Siku hizi vijana hawataki kutumia akili nyingi, hawataki kutumia nguvu. Wanataka maisha rahisi, walelewe. Wakiwa na familia jukumu la malezi wanaliacha kwa mwanamke. Unakuta  mwanamke anaamka alfajiri anakwenda sokoni ananunua maembe anaweka kwenye beseni anatembeza barabarani anauza, mwanaume anaamka saa tano, anataka akute chai mezani akinywa anaishia kijiweni,” alisema.

Fransisca Peter mkazi wa Tegeta, Dar es Salaam, ambaye ni mama mwenye watoto watatu wakiwamo wawili wa kiume, alikiri kwamba wazazi wengi wamesahau malezi na kufanya watoto wajilee kupitia mitandao ya kijamii matokeo yake yanaonekana hivi sasa.