GCLA yapongezwa utoaji wa ripoti za uchunguzi kwa wakati

30Jan 2024
Mary Geofrey
Nipashe
GCLA yapongezwa utoaji wa ripoti za uchunguzi kwa wakati

MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), imepongezwa kwa kuimarisha utoaji wa ripoti za uchunguzi wa kimaabara za mashauri mbalimbali kwa muda mfupi.

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo (kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi wa Huduma za Sayansi Jinai wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), David Elias, aliyekua akimpa maelezo wakati Kamishna huyo alipitembelea Banda la Mkemia Mkuu katika maonyesho ya Wiki ya Sheria Kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma.

Pongezi hizo zimetolewa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, David Ngunyale, katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria, Kanda ya Dar es Salaam.

Amesema utoaji wa ripoti za uchunguzi wa vinasaba kwa sasa umeimarika tofauti na hapo zamani.

“Hongereni sana utoaji wa ripoti za uchunguzi wa vinasaba kwa sasa umeimarika sana, kwa sasa ripoti zinatoka mapema ukilinganisha na hapo zamani. ”amesema Jaji Ngunyale.

Naye Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Salma Maghimbi, ameipongeza mamlaka kwa utendaji kazi uliotukuka huku akiishukuru mamlaka kwa ushiriki wake katika maadhimisho hayo kama wadau muhimu katika mnyororo wa haki.

“Hongereni sana kwa kazi nzuri na nzito mnayoitoa kwa jamii na tunawashukuru sana kwa ushirikiano wenu katika maadhimisho haya,”amesema Jaji Maghembe.

Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yalianza Januari 24, 2024 na yanatarajiwa kuhitimishwa Februari 1, 2024.