Feza kusomesha bure wanafunzi

03Apr 2016
Beatrice Shayo
Nipashe Jumapili
Feza kusomesha bure wanafunzi

ILI kuhamasisha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi uongozi wa shule ya Feza, umeandaa mashindano ya kuwaibua wenye vipaji pamoja na kuwapatia ufadhili wa kusoma bure.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkuu wa shule ya Sekondari ya Feza, Ibrahimu Yunus, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuwatangaza washindi waliofanya vizuri katika masomo ya sayansi.

Alisema lengo la mashindano hayo ni kuwapa hamasa ya kupenda kusoma masomo ya sayansi ili kulikwamua taifa na tatizo la kutokuwa na wataalamu katika sekta hiyo.

Yunus alisema mashindano hayo yamefanyika kwa mikoa 10 kwa shule ambazo zipo karibu na Feza na kwa washindi watatu wamepatiwa zawadi.

“Lengo letu ni kuibua vipaji katika shule mbalimbali za nchini hasa katika masomo ya sayansi," alisema na kueleza zaidi kuwa "kuna wengine wana uwezo wa kusoma lakini hawafikii malengo yao.

"(Hivyo) wanafunzi hawa tunawachukua na kuwasomesha bure na hata kuwapeleka nje ya nchi kusoma zaidi.”
Wanafunzi wengi walijitokeza kufanya mitihani "tuliyowaandalia, kwa ujumla ni wanafunzi 3,000 na kwa Dar es Salaam (pekee) ni wanafunzi 400.”

Alisema mbali na kuwasomesha shuleni hapo wapo wanafunzi wengine 180 ambao huwapatia sh. 250,000 kwa kila mwaka kupitia shule wanazozisoma ili wasome katika mazingira mazuri.

Aidha, Yunus alisema tangu waazishe programu ya kuwasaidia wanafunzi kila mwaka ni zaidi ya wanafunzi 200 ambao husoma bure katika shule za Feza.

Yunus alisema wamejipanga kusaidiana na wizara ya elimu katika kuwawezesha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi ili kuwepo na ongezeleko la wataalamu katika nyanja hiyo.

“Haya mashindano ni mazuri hata mimi nimeibuliwa kwenye hizi shule za kayumba nikafanikiwa kusomeswa na shule ya Feza hadi kufikia kuwa Mkuu wa shule.”