Ebola yaua daktari Mtanzania Uganda

02Oct 2022
Na Waandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Ebola yaua daktari Mtanzania Uganda

SIKU tatu baada ya serikali kutangaza tahadhari ya ugonjwa wa ebola nchini, daktari bingwa wa kitanzania aliyekuwa Uganda, amefariki dunia, Wizara ya Afya imethibitisha.

Dk. Mohamed Ali Hafidh.

Ni tukio linalochukua sura huku kukiwapo hatua za kiserikali za tahadhari, kuletwa maabara tembezi, operesheni ya elimu kwa umma na angalizo maalum kwa mikoa iliyo jirani na kulikoathirika.

Taarifa ya wizara hiyo iliyotolewa jana jioni, ikitiwa saini na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na Waziri mwenzake wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Nassor Mazurui, ilitamka:

“Tarehe moja (jana) Wizara ya Afya, imepokea taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ikitoa taarifa ya kifo cha Dk. Mohamed Ali Hafidh aliyekuwa akisomea udaktari bingwa wa upasuaji Uganda akitokea Tanzania.”

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tangu mwezi uliopita katika  wilaya nne za Uganda, zimeshapata wagonjwa 54 wa maradhi hayo na kati yao, 25 walifariki dunia.

“Tarehe 28 mwaka huu, tulitoa tamko la kuupa habari umma pamoja na kutoa tahadhari kuhusu ugonjwa huu kwa wananchi ikiwamo hatua za kuchukua ili kujikinga,” ilisema.

Juzi jioni kwenye mjadala wa redio moja ya nje, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi alitaja hatua zinginezo ni serikali inaendelea na kampeni za kuelimisha umma ngazi ya chini kuhusu ugonjwa huo katika mikoa iliyoko hatarini zaidi, ukiwamo wa Kagera.

Vilevile, jana serikali ilitangaza kuweka maabara tembezi ya kupima virusi vya ebola katika Kituo cha Afya Kabyaire wilayani Misenyi, Kagera ambako ni mpakani na Uganda.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dk. Issessanda Kaniki, alisema mjini Bukoba kwamba serikali imeweka maabara hiyo tembezi kusaidia kupima virusi vya ebola, akitaja kwenye Kituo cha Afya Kabyaire.

Katika kikao na wadau wa afya cha kujadili mlipuko wa ebola, alisema kuna hospitali 12 zitakazotoa huduma ya matibabu ya ebola, yakiwa yametengwa maeneo maalum kwa ajili ya kutoa huduma wagonjwa hao katika vituo vyote vya afya mkoani humo.

“Mashine iliyofungwa kituo cha Kabyaire, baada ya mtu kupimwa virusi vya ebola, majibu yanatoka ndani ya saa mbili na wameletwa wataalamu wa afya wanne katika kituo hicho,” alifafanua.

Dk. Kaniki alisema baada ya mtu kupimwa na kuonekana na dalili, kutakuwa na gari la wagonjwa kwa ajili ya kuwasafirisha kwenye vituo maalum.

Alisema kila halmashauri imetenga eneo la karantini kwa ajili ya kuwaweka washukiwa wa ebola na watoa huduma.

*Imeandaliwa na Romana Mallya (DAR) na Mary Geofrey (Kagera.