Agizo hilo alilitoa jana katika kikao cha wadau wa afya mkoani hapa, ambacho kilihudhuriwa na ujumbe kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), kilichokuwa na lengo la kujadili mlipuko huo.
Gallawa alisema viongozi wamelikumbatia suala la kipindupindu wenyewe bila ya kutoa elimu kwa jamii juu ya namna ya kupambana nao.Alisema hadi kufika Machi 15 kusiwe na mgonjwa yeyote wa kipindupindu mkoani humo.
“Niliagiza kamati za afya kila kata zipite mtaani na kukagua vyoo na usafi wa mazingira kwa ujumla kila siku asubuhi lakini nasikitika hili halijafanyika maana lingefanyika hawa asilimia 40 wasio na vyoo wangesukumwa na kuvijenga,” alisema Gallawa.
Aidha, Gallawa alisema kutokana na viongozi kutowajibika ipasavyo kupambana na ugonjwa huo, ndiyo maana mlipuko huo bado upo Dodoma.
“Viongozi kuanzia ngazi ya vitongoji hadi wilaya simamieni suala la usafi wa mazingira katika maeneno yote, ikiwemo yale yanayofanyika biashara mbali mbali ili kuhakikisha taratibu zote za usafi zinafuatwa,” alisema Mkuu huyo.
Aliagiza kila kiongozi lazima ahakikishe anatoa taarifa kwa wananchi juu ya kurudi kwa ugonjwa huo na kudhibiti biashara zote zinazoweza changia kuenea kwake, ikiwemo kuzuia uuzaji na utengenezaji wa pombe za kienyeji.
“Fungeni baa na vilabu vyote vya pombe za kienyeji ambavyo havitazingatia sheria na taratibu za usafi ikiwa ni sehemu ya kuzuia usambaaji wa vimelea vya ugonjwa wa kipindu pindu,” alisema.
Naye Mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa Dodoma, Dk. Nassor Mzee aliwashauri viongozi wa halmashauri za wilaya kuwa na maazimio ya mapambano dhidi ya kipindupindu katika maeneo yote na kuhakikisha wanazungumza na wananchi ili wazingatie kanuni za afya.
Mwakilishi wa WHO nchini, Rufaro Chatora, aliwataka viongozi kuacha kutumia mabavu wakati wanashughulikia tatizo la kipindu pindu na kwamba wananchi wanapaswa kupewa elimu.
Tangu ugonjwa huo uingie mkoani hapa Agosti mwaka jana, jumla ya wagonjwa 639 wameugua na 18 kati yao wamepoteza maisha.









