Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kiongozi huyo kufanya ziara ya kushtukiza shuleni huko. Shule hiyo inachukua wanafunzi wa jamii ya wafugaji wa kimasai.
Shaka alifika shuleni kuona idadi ya wanafunzi waliopokewa tangu Januari 8, mwaka huu, shule zilipofunguliwa.
Alisema shule hiyo imepangiwa wanafunzi wa kidato cha kwanza 59. Kati yao, wasichana ni 29, lakini walioripoti hadi siku ya pili baada ya shule kufunguliwa, walikuwa ni watano tu (wote wa kiume).
Shaka alisema kuwa wiki mbili kabla ya shule kufunguliwa kuanza mwaka mpya wa masomo, alipokea kesi mbili katika kata hiyo za wazazi ambao wamepokea ng’ombe ili kuwaozesha mabinti zao kabla ya matokeo kutangazwa.
Mkuu wa Wilaya alisema kesi nyingine ilihusu mtoto wa kike ambaye wazazi wake wametorosha kwa ujanja, wakidai ni mgonjwa, lakini ufuatiliaji ukabaini alipelekwa kwa mganga wa kienyeji.
"Binti siyo kwamba anaumwa, bali alipelekwa kwa mganga kimkakati kwa maana ya wazazi wanavuta muda ili baadaye waweze kwenda kumfugisha ndoa," alisema Shaka.
Pia alisema baadhi ya wazazi wamewapeleka kimkakati watoto wao wa kike mjini Morogoro katika shule ambazo hazijasajiliwa ili baadaye wawarudishe na kuwaozesha.
"Kuanzia sasa serikali tutakuwa wakali sana, hatutasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa mzazi yeyote atakayebainika kwa namna moja ama nyingine anamhujumu mtoto wake katika suala la kupata elimu," alisema.
Shaka aliwaagiza viongozi wa kata pamoja na diwani kuwafuatilia, hasa wa kike, ili kujua waliko kwa kuwa kuna tabia zilizojengeka za baadhi ya wazazi kuwatorosha watoto wao wa kike waliofaulu darasa la saba na kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza.
"Lengo ni tujue wako wapi? Je, wapo ndani ya jamii ya Parakuyo au wamepelekwa maeneo mbalimbali? Kama ndivyo, tuchukue hatua dhidi ya wazazi wao,” alisema.
Diwani wa Parakuyo, Ibrahimu Kalaita, alisema bado ni mapema kujua watoto wa kike waliochanguliwa kujiunga kidato cha kwanza shuleni huko kama wamechepushwa au la.
"Ninajua muda uliowekwa kisheria bado na wazazi wanaendelea kujindaa kuwaleta watoto shuleni, lakini sisi viongozi wa kata tutaendelea kutekeleza maelekezo ya Mkuu wa Wilaya," alisema Kalaita.
Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, ambayo mwaka jana ilifanyiwa mapitio, sasa inaelekeza elimu ya msingi na sekondari kidato cha kwanza hadi cha nne ni ya lazima.










