Wito huo ulitolewa kupitia taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya Prof. Pascal Ruggajo kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu iliyolenga kutoa taarifa ya uchunguzi wa awali ya ugonjwa huo.
Prof. Ruggajo alisema dalili ya ugonjwa huo ni pamoja na macho kuwasha, kuchoma choma, kuuma, kutoa machozi na tongo tongo za njano, hali ambayo inaripotiwa kuonekana kwa baadhi ya watu nchini.
“Taarifa za uchunguzi zinaonyesha maambukizi ya kirusi hiki kwenye ngozi ya juu ya gololi ya jicho ni maambukizi yanayosambaa kwa kasi kubwa. Hakuna tiba maalumu kwa ugonjwa huu na hata bila tiba dalili huisha zenyewe ndani ya wiki mbili,” alisema Prof. Ruggajo.
Aliongeza kuwa mwenendo wa ugonjwa huo unaonyesha kuna ongezeko kubwa la wagonjwa wanaofika katika vituo vya kutolea huduma za afya wakiwa wanasumbuliwa na ugonjwa huo.
“Katika kipindi cha Desemba 22, 2023 hadi Januari 11, mwaka huu kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaosumbuliwa na ugonjwa huu kufika katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya matibabu, kwa mfano katika mkoa wa Dar es Salaam kuna wagonjwa wapya 869 huku hali ya kawaida katika kipindi cha mwezi Desemba 2023 kulikuwa na wagonjwa 17 pekee,” alisema Prof. Ruggajo.
Aidha, alisisitiza kuwa suala la usafi ni jambo muhimu katika kuzuia maambukizi kusambaa kwa wengine kutokana na tabia ya ugonjwa huu kusambaa kwa kasi, na kwamba maambukizi hayo huleta mlipuko ambao husambaa kupitia kirusi kwa asilimia zaidi ya 80.
Hata hivyo aliwashauri wananchi kutokutumia dawa zisizo rasmi na ambazo hazijaandikwa na daktari kwa wakati huo na kutotumia dawa za macho anazotumia mgonjwa mwingine ili kuepuka madhara kwa kuwa dawa za macho ni tofauti na zinatolewa kwa matumizi tofauti.










