Daktari auwawa kisha kuporwa pikipiki

07May 2023
Samson Chacha
TARIME
Nipashe Jumapili
Daktari auwawa kisha kuporwa pikipiki

DAKTARI Isack Daniel wa Kituo cha Afya Kerende katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, ameuawa kwa kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili kisha wauaji kupora pikipiki yake.

DAKTARI Isack Daniel.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Kamishna Msaidizi (ACP) Geofrey Sarakikya, alisema juzi kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Mei 4, mwaka huu.

ACP Sarakikya alisema baada ya watu hao kutekeleza mauaji hayo, waliutelekeza mwili wa daktari pembezoni mwa barabara.

Alisema mwili huo ulitambuliwa na wananchi baada ya kumkuta tayari amefariki dunia akiwa na majeraha katika maeneo mbalimbali ya mwili pamoja na kitu chenye ncha kali pembeni mwake.

Pia alisema wananchi hao pamoja na wanafamilia wa marehemu, walilieleza Jeshi la Polisi kuwa wakati wa tukio hilo, Dk. Daniel alikuwa na pikipiki ambayo iliporwa na watu hao.

“Tunaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na kifo cha daktari huyo na tunaendesha msako ili kubaini kila mmoja aliyehusika na uhalifu huu. Tunawaomba pia wananchi kutoa ushirikiano kwa kuwafichua wahalifu hao ili sheria ichukue mkondo wake," alisema.

Diwani wa Kemambo, Rashid Bogomba, alisema kutokea kwa tukio hilo la mauaji kumesababisha pengo kwa wakazi wa eneo hilo kutokana na daktari huyo kuwa na mchango mkubwa katika kutoa huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo.

Diwani huyo alilaani tukio hilo na kuliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi na kuwabaini mapema wahusika ili kuondoa hofu ambayo imetanda kwa wakazi wa kata hiyo.