Kampuni hiyo ya uwakili inadaiwa irejeshe Sh milioni 21 za mjane Brigitte Ringia na watoto wake watatu ambao ni Warren David Lyimo (16), Davina David Lyimo 5 na Noah David (7), fedha ambazo ni sehemu ya Sh. milioni 54 alizolipwa mume wa mjane huyo aitwaye David Lyimo kwenye kampuni ya Chinese-Tanzanian Joint Shipping Company, ikiwa ni fidia baada ya kuumia kazini.
Akizungumza na gazeti hili bila kutaja jina lake, mmoja wa wanasheria wa chama hicho alisema familia hiyo inapaswa kuwasilisha malalamiko yake kwa maandishi ili TLS iweze kusikiliza maelezo ya pande hizo mbili na kisha ijue hatua za kuchukua.
Alisema chama hicho kikishapata mamamiko rasmi kitaita upande unaolalamikiwa kusikiliza maelezo yake na kama itabainika kuwa kampuni hiyo ilichukua fedha hizo bila kuwa na makubaliano na familia ya marehemu David ataamliwa kuzirejesha.
“Wanapaswa kutuletea malalamiko yao kwa maandishi tukiona yana msingi na kama zile hela zilichukuliwa kimakosa basi kamati ya nidhamu ipo na hatua stahiki zitachukuliwa ili familia ipate haki yake….tutachunguza kupata ukweli,” alisema.
David ambaye alikuwa mume wa Brigitte alifariki mwaka 2009, baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana waliompiga risasi zilizosababisha umauti wake.
Kwa mujibu wa msimamizi wa mirathi ya marehemu David, Fritz Msanjo, ambaye ni kaka wa marehemu, kampuni ya Ngalo ilikuwa ikisimamia kesi ya madai namba 239 ya mwaka 2003 , ambapo David alikuwa akiidai kampuni ya Chinese alikokuwa akifanyakazi na kuumia.
Kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Samora jijini Dar es Salaam.
Ndugu wa marehemu huyo walisema ni kweli kuwa awali ndugu yao alikuwa akiwakilishwa na kampuni ya Ngalo mahakamani lakini baada ya kugunudua kuwa huwa hafiki mahakamani mara nyingi aliamua kuiandikia barua mahakama ya kumkataa.
Barua ya David kwa mahakama, ambayo nakala yake tunayo ilisema kuwa yeye David kwa hiyari yake ameamua kuchukua uamuzi wa kujisimamia katika kesi yake ya madai dhidi ya kampuni ya meli ya China baada ya kuona wakili wake hahudhurii kesi yake.
Msanjo alisema marehemu David aliendelea kujisimamia mwenyewe mahakamani hadi alipofariki muda mchache kabla ya hukumu kutoka ndipo walishangaa kuona kampuni ya uwakili ya Ngalo imechukua fedha hizo na kuzigawa badala ya kuzipeleka mahakamani.
Alisema fedha hizo ilipaswa zipelekwe mahakamani ili zigawiwe lakini alikiuka utaratibu huo kwa makusudi na kujichotea Sh. milioni 21 kisha Sh. milioni 33 zilizobaki kuingiza kwenye akaunti ya mjane wa marehemu ambaye wakati huo hakuwa anajua kiasi kilichotolewa na mwajiri wa marehemu.
“Cha ajabu zilipotoka zile milioni 54 kutoka kwenye ile kampuni ya meli, Ngalo alizipitishia zile fedha kwenye akaunti yake na kuchota milioni 21 na zilizobaki akampa mjane na mjane alichukua zile fedha bila kujua kuwa fedha zilizotolewa na ile kampuni ya meli ni kiasi gani “ alisema Msanjo
Alisema hata kama Ngalo angekuwa ndiye msimamizi wa kesi ile hakupaswa kulipwa kiasi hicho kikubwa cha fedha kwani sheria inataka mtu anayesimamia shauri kama hilo alipwe asilimia tatu tu ya fedha zitakazolipwa baada ya kesi kumalizika na kama hilo lingezingatiwa basi kampuni ya Ngalo ingestahili kulipwa Sh. milioni tatu.
“Tunamwomba Ngalo arejeshe fedha za mjane na watoto ili ziwasaidie katika kuendesha maisha yao….huu si ubinadamu mtu kuchukua fedha za watu wanyonge wasioweza kujitetea, watoto wale wanamahitaji mengi kama shule na malazi, yeye anadai alikubaliana na marehemu lakini hajawahi kutuonyesha na wala hawezi kuonyesha waliandikiana wapi,” alisema.
Alisema iwapo David angekuwa hai na zikatoka hizo milioni 54 zingekwenda moja kwa moja kwenye akaunti yake hivyo hakukuwa na uwezekano wowote kwa kampuni ya uwakili kulipwa kiasi kikubwa cha fedha kama alizojilipa Ngalo.
“Fedha za mirathi zinagawiwa mahakamani sasa yeye ndiye Mahakama? Alichukua jukumu la kugawa fedha za mirathi yeye kama nani? Tunamwomba kama ana nia njema azipeleke hizo fedha mahakamani ili zigawiwe kwa watoto wa marehemu,” alisema Msanjo.
Kampuni ya uwakili ya Ngalo iliiandikia barua Hakimu Mfawidhi, Mahakama ya Mwnazo Kawe, ikijitetea kuwa kampuni yake ilisimamia kesi ya Davidi dhidi ya mwajiri wake kwa madhara aliyoyapata akiwa kazini.
Alisema wakati wanakubalia kumuwakilisha katika kesi hiyo, marehemu David alikuwa hana uwezo wa kifedha kwani aliwaeleza kuwa ana madeni mengi kutokana nna gharama za kujitibu na kuielea familia yake.
“Tuliisimamia na kuendesha kesi yake bila kuchukua malipo yoyote kwake isipokuwa gharama za kufungulia shauri na kwa kuzingatia hali yake wakati ule, tulisukumwa na utu na ubinadamu ili kuhakikisha anapata haki yake kwanza ….tulikuwa na maelewano naye kuwa tufanye kazi na tukifanikiwa atatulipa staili yetu na shukrani kwa kujitolea kwetu,” ilisema sehemu ya utetezi wa kampuni ya uwakili ya Ngalo.
Ngalo mwenyewe alisema kiasi alicholipwa yalikuwa makubaliano halali baina yake na marehemu kwamba amsimamie kesi yake bila malipo kwa kuwa hakuwa na fedha wakati huo lakini atakapolipwa atampa sehemu ya malipo hayo waliyokubaliana.
“Yule mjane wa marehemu anajua mchakato mzima wa namna nilivyomwakilisha mumewe mahakamani wakati akiwa hana hela, nilifuatilia kesi mahakamani hadi hukumu ilipotoka na fedha nilizompa na nilizobaki nazo mimi tulikubaliana na si kwamba niliamua mwenyewe,” alisema.
Aidha, Ngalo alisema kama kuna ndugu wa marehemu anayeona yeye (Ngalo) hakuwa na uhalali wa kupata fedha hizo basi apeleke shauri hilo katika Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), ambapo kuna kamati ya maadili inayosimamia wanasheria.
“Haya mambo yako wazi mimi sijala hela ya mtu kama wanaona hizi fedha hazikuwa halali yangu waende kwenye kamati za maadili za Chama Wanasheria Tanganyika (TLS) huko nitatoa ushahidi wangu, kwenye chama mtu anayelalamika kwamba mtu ametapeliwa ama ameibiwa anasikilizwa ” alisema wakili huyo.
Chama cha wanasheria chaingilia kati milioni 21 za mjane
06Feb 2016
Mary Geofrey
Nipashe
Chama cha wanasheria chaingilia kati milioni 21 za mjane
CHAMA cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kimeingilia kati suala la milioni 21 zilizochukuliwa na kampuni ya uwakili ya Ngalo & Company Advocates ya jijini Dar es Salaam, na kuahidi kufuatilia suala hilo kwa karibu ili kujua ukweli wake.










