Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Tanzania Bara, Benson Kigaila, alitoa rai hiyo wakati akitangaza kusogezwa mbele kwa maandamano hayo yaliyotarajiwa kufanyika Februari 13, mwaka huu kutokana na uwanja kuwa na matumizi mengine.
Kigaila alisema maandamano hayo ya awamu ya pili yatafanyika katika barabara za Jiji la Mwanza na kuhitimishwa kwenye Viwanja vya Furahisha kwa mkutano na wananchi utakaohudhuriwa na viongozi wote wa CHADEMA kitaifa.
"Maandamano ya Mwanza si ya CHADEMA tu, bali ni ya watanzania wote wanaokerwa na ugumu wa maisha. Hivyo, tunawaita wana CCM waje tushirikiane kuidai serikali kuja na mpango madhubuti wa kudhibiti ugumu huu kwani kwa sasa wote tunaisoma namba," alisema Kigaila.
Alisema wanaendelea vizuri na maandalizi na taarifa ya maandamano tayari imepelekwa kwa wakuu wa polisi ngazi za wilaya yatakakofanyika maandamano hayo kwa mujibu wa sheria.
"Tayari tumewajuza polisi siku saba kabla ya maandamano licha ya sheria kututaka kuwasilisha taarifa ndani ya siku mbili, hivyo tumewaahidi zaidi na tunatarajia kuwa na njia tatu za maandamano ambazo zitaungana katika eneo la Bustani ya Grand-Hall kisha kuelekea katika Viwanya vya Furahisha," alisema Kigaila.
Alisema ajenda za maandamano hayo ni zilezile za kuishinikiza serikali kupitia Rais Samia Suluhu Hassan kutokutia saini miswada mitatu ya sheria zinazohusiana na uchaguzi zilizopitishwa na Bunge hivi karibuni kwa kuwa "haijasikiliza maoni ya wananchi".
Alitaja ajenda ya pili ni kushinikiza serikali kuchukua hatua za makusudi kudhibiti mfumuko wa bei unaosababisha ugumu wa maisha na kupanda kwa gharama za vitu mbalimbali ikiwamo sukari, nauli na mafuta.










