Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, aliyasema hayo juzi jijini hapo wakati wa kongamano la BAWACHA la kudai Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi na kwamba baraza hilo ni nguzo kubwa kwenye mchakato huo.
Alisema kwa sasa nchi nzima watu wanazungumzia Katiba Mpya, lakini kuna wasiwasi kwamba kipengele cha Tume Huru kinaweza kikasahaulika kwa kufunikwa na mambo mengine au kuhujumiwa na watu wasiolitakia mema taifa.
Mnyika alidai baadhi ya viongozi wa serikali pamoja na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi wamekuwa wakizungumza kwenye vyombo vya habari wakionyesha kukubaliana na mchakato wa Katiba Mpya, lakini hawana nia njema kama inavyofikiriwa.
Alisema viongozi hao wamekuwa wakisisitiza kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya kwa kuanzia na Katiba Pendekezwa ambayo alisema ilishachakachuliwa na kutaka mchakato uanzie kwenye Katiba ya Tume ya Jaji Joseph Warioba.
Alisema Tume Huru ya Uchaguzi ndiyo msingi wa uongozi bora na imara wa taifa na lazima kila Mtanzania mwenye nia njema aipiganie na chama hicho kimekabidhi jukumu hilo kwa BAWACHA.
Alisema Katiba Pendekezwa ambayo viongozi wa CCM wanaitaka bado ina mwendelezo wa Tume ya Uchaguzi kuteuliwa na Rais pamoja na kuapishwa na Rais na endapo mchakato huo utaendelea kuna hatari ya kipengele hicho kuhujumiwa.
“Katiba pendekezwa mbali na kumpa Rais mamlaka ya kuteua na kuapisha Tume ya Uchaguzi, pia imempa mamlaka ya kuteua mpaka Mkurugenzi wa Tume na makamishna, sasa hii haina tofauti kabisa na hii ya mwaka 1977,” alisema Mnyika.
Alisema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 CHADEMA pamoja na vyama vingine vya upinzani vilihujumiwa kutokana na ubovu wa muundo wa Tume ya Uchaguzi.
Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa, aliwataka wanawake wa chama hicho kuchangamkia fursa ya kugombea ubunge kwenye majimbo ya uchaguzi utakapofika badala ya kutegemea viti maalumu pekee.
Msigwa alisema viti maalumu pekee havisaidii kundi hilo kuwa na uwakilishi mzuri kwenye Bunge kwa kuwa hata kama chama hicho kitashinda majimbo yote nchini bado wanawake wa viti maalumu hawawezi kuzidi 130.
Aliwataka wanawake wa chama hicho kuhakikisha wanajikita katika shughuli mbalimbali zikiwamo za kiuchumi na kijamii ili kukijenga chama katika misingi ya kuwa mbadala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho alisema kimeshindwa kuiendesha serikali,” alisema Msigwa.
Alisema serikali imeshindwa kutatua matatizo ya wananchi ikiwamo ukosefu wa ajira kwa vijana, tatizo la maji na mfumuko wa bei za vitu na kuwataka wanawake wa chama hicho kuwasemea wananchi kwenye majukwaa mbalimbali.










