CHADEMA, CCM waungana kumuaga Masinde

19Mar 2023
Vitus Audax
Mwanza
Nipashe Jumapili
CHADEMA, CCM waungana kumuaga Masinde

MWENYEKITI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Freeman Mbowe ameongoza mamia ya wanachama wa chama hicho pamoja na waamini wa Kanisa Katoriki katika ibada ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini na muasisi wa chama hicho, Silvester Kanyasu Masinde iliyofanyika jana.

Ibada hiyo ilifanyika katika Kanisa Katoliki la Parokia ya Watakatifu Petro na Paulo Mwananchi iliyopo Kata ya Mahina Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza iliyoudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho wakiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe pamoja, John Mnyika,John Heche,Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini Maulida Komu na viongozi wengine wa chama hicho na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi CCM aliyemuwakilisha mwenyekiti wa Chama hicho.Akizungumza katika ibada hiyo,Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Freeman Mbowe alisema chama hicho kimapoteza mtu muhimu na mwalimu wa muda wote wa viongozi na wanachama.

Alieleza kuwa CHADEMA kimepoteza Maktaba yenye uwezo mkubwa wa akili katika kuandaa na kuandika vitabu na makala mbalimbali kudai haki, amani na maendeleo kwa manufaa ya chama na Taifa kwa ujumla.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti Mbowe, alitoa pongezi zake kwa Mwenyekiti wa Chama Cha mapinduzi CCM kwa kutoa ruhusa kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM Mohamed Ali Mohamed kushiriki katika ibada hiyo ya kumuaga mpendwa wao.Aliwasilisha salamu za rambirambi kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Taifa, katika ibada hiyo Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM Mohamed Ali Mohamed  alisema chama hicho kitakuwa pamoja na wanafamilia na wanachama wa CHADEMA katika kipindi hiki cha majonzi kwa kuwafariji bila kujali tofauti zao za kiitikadi.

Silvester Masinde alifariki Dunia Machi 15 mwaka huu katika Hospitali ya Rufani Kanda Bugando alipokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa Saratani ya Tezi Dume.