Bodaboda wampiga Luteni wa JWTZ, azimia

27Mar 2016
Gideon Mwakanosya
Nipashe Jumapili
Bodaboda wampiga Luteni wa JWTZ, azimia

POLISI mkoani Ruvuma inawashikilia waendesha bodaboda 20 wa Manispaa ya Songea kwa tuhuma za kumpiga mawe na kumjeruhi askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), abiria aliokuwa nao na kuharibu gari lake.

Mkuu wa Majeshi Nchini Jenerali Davis Mwamunyange

Askari huyo Samueli Nginila (32), alipata kipigo baada ya kumgonga mtembea kwa miguu, kwa mujibu wa Kamanda Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Zuberi Mwombeji.

Akizungumza na wanahabari alisema tukio hilo lilitokea Alhamisi wiki hii saa tatu usiku maeneo ya Shule ya Msingi Mfaranyaki iliyo karibu na kitu kikuu cha polisi Songea Mjini.

Alieleza kuwa askari alijeruhiwa kwa kushambuliwa sehemu mbalimbali na waendesha bodaboda na kwamba anafanyakazi kikosi cha 411 KJ cha Ruhuwiko ambako kwa sasa hivi amelazwa katika hospitali ya serikali ya mkoa wa Songea (Homso) kwa matibabu zaidi.

Alifafanua zaidi kuwa inadaiwa siku hiyo Nginila alijeruhiwa sehemu mbalimbali na kupoteza fahamu baada ya kushambuliwa na waendesha bodaboda ambao walivunja vioo vya gari kwa kuvipiga mawe.

Alisema chanzo cha tukio hilo ni ajali iliyotokea maeneo ya Majengo ambako Nginila akiwa na gari namba T 967 DAE aina ya Nissan Xtrail akitokea kwenye baa alimgonga Bahati Mbero, akiwa anakatisha ghafla na kupata majeraha madogo.

Alieleza zaidi kuwa katika tukio hilo madereva wa bodaboda waliokuwa karibu na eneo la ajali walikusanyika na kumshambulia dereva wa gari hilo aliyelazimika kuwasha gari na kukimbia ili kuokoa maisha yake na baadaye madereva wa bodaboda walimkimbiza ili kumshambulia.

Lakini, Nginila alipofika maeneo ya Shule ya Mfaranyaki alishindwa kukimbia kwani moja ya matairi ya gari yake lilichomoka na baadaye madereva walimzingira na kumshushia kipigo cha mawe pamoja na abiria watatu aliokuwa nao.

Aliwataja waliopigwa kuwa ni Kaumbya Kateka (24) mkazi wa Majengo, Joyce Edson (24) anayeishi Mpambalyoto na Jackline Mwita (22) mwanafunzi wa Chuo cha Uuguzi Peramiho wilaya ya Songea Vijijini ambao walikimbizwa hospitalini ,kutibiwa na kuruhusiwa.

Aidha Kamanda Mwombeji alisema katika vurugu hizo baadhi ya mali za Nginila zilipotea ambazo ni simu mbili za mkononi, pochi ambayo ilikuwa imehifadhi vitambulisho vya kazi, kupigia kura, kadi za benki pamoja na Shilingi 120,000.