Biteko akoleza moto maoni miswada sheria ya uchaguzi, vyama vya siasa

03Jan 2024
Na Mwandishi Wetu
GEITA
Nipashe
Biteko akoleza moto maoni miswada sheria ya uchaguzi, vyama vya siasa
  • Asema Rais, Dk. Samia anafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha watanzaia
  • Ataka Wananchi kuchagua viongozi bora katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amewahimiza Watanzania kushiriki kutoa maoni kuhusu muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2023.

Miswada mingine ambayo iliwasilishwa bungeni Novemba, mwaka jana, na wananchi kutakiwa kutoa maoni ni wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa mwaka 2023 na wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa mwaka 2023.

 

Kwa kufanya hivyo, Biteko amesema ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Rais  Samia Suluhu Hassan za kujenga Tanzania iliyo bora zaidi katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Dk. Biteko amesema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mbogwe mkoani hapa katika sherehe za kuaga mwaka 2023 na kuukaribisha mwaka 2024 zilizoandaliwa na Mbunge wa Mbogwe, Nicodemus Maganga, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali mkoani Geita wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Martine Shigella.

“Rais amepeleka miswada hii bungeni iliyosomwa wakati wa Mkutano wa 13 wa Bunge na tangazo limeshatoka la kuwaomba wananchi kwenda kutoa maoni yao bungeni kuanzia Januari 6 hadi 10, 2024 kuhusu marekebisho ya sheria hizi. Niwaombe Watanzania nendeni mkatoe maoni yenu ili kujenga Tanzania iliyo bora kuliko kubaki nyuma kulalamika,” alisisitiza.

Dk. Biteko alisema Rais Samia anafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha Watanzania wa vyama, dini na makabila mbalimbali na anasikiliza malalamiko ya makundi mbalimbali na kuyafanyia kazi. Alitoa mfano wa  suala la kuruhusu vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara ili kueleza sera zao na kwamba nia ya Rais ni kujenga mshikamano na umoja nchini.

Kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika baadaye mwaka huu, Dk. Biteko aliwahimiza wananchi kuchagua viongozi bora na kwamba watu wasigawanyike na kufarakana kwa sababu ya uchaguzi bali waungane kwa kuzungumza  yanayowaunganisha kama vile barabara, maji, umeme na wasiruhusu mtu kupandikiza chuki kati yao.

Katika salamu zake za Mwaka Mpya, Biteko aliwasisitiza Watanzania kupendana, kuthaminiana, kuvumiliana, kusameheana, kuwa na shukrani, kusaidiana na kumfanya mtu mwingine afurahi, lengo likiwa ni kujiletea maendeleo.

Kuhusu hali ya upatikanaji umeme wilayani Mbogwe, Dk. Biteko alisema itaendelea kuimarika kwa kuwa imejengwa njia mpya ambayo itapeleka umeme wilayani humo kutokea kituo cha Nyakanazi. Pia alisema itajengwa njia nyingine ambayo itapeleka umeme Mbogwe kutokea Kahama pamoja na kituo cha kupoza na kusambaza umeme wilayani humo.

Awali, akiwasilisha salamu za Mwaka Mpya, Shigella alisema anaridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye Wilaya ya Mbogwe ikiwamo elimu, maji, umeme, barabara na afya.

Kuhusu utekelezaji wa miradi ya umeme mkoani Geita, Shigella alisema asilimia 90 ya vijiji vya mkoa huo tayari vimeshapatiwa umeme na vijiji 50 vilivyosalia kazi za kusambaza zinaendelea ikijumuisha mipango ya kupeleka umeme hadi kwenye vitongoji.

 

Naye Mbunge wa Mbogwe, Maganga, alimshukuru Naibu Waziri Mkuu  kwa kufika Mbogwe kushiriki na wananchi katika sherehe hizo na kuongeza kuwa Mbogwe imejipanga kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwamo sekta ya madini kuendelea kufanya vizuri.