Bil. 3/- zatolewa ujenzi wa shule ya sekondari 

04Sep 2022
Gideon Mwakanosya
Namtumbo
Nipashe Jumapili
Bil. 3/- zatolewa ujenzi wa shule ya sekondari 

SERIKALI imetoa Sh. bilioni tatu kutekeleza mradi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Mkoa wa Ruvuma ambayo inajengwa katika eneo la Migelegele wilayani Namtumbo.

Akizungumza baada ya kukagua mradi huo jana, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Laban Thomas, alisema ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo, shule hiyo ikitarajiwa kuanza kudahili wanafunzi  mwakani.

Kanali Laban alisema Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa 10 ambayo serikali imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule maalum za sekondari za wasichana za mikoa.

“Mheshimiwa Rais anatafuta fedha kuhakikisha miradi mbalimbali inatekelezwa ukiwamo mradi huu wa sekondari za wasichana, ninawapongeza wote kwa kujitoa kusimamia kuhakikisha mradi huu unakamilika," alisema.

Kanali Thomas alisema kuna baadhi ya mikoa inayotekeleza mradi huo haijaoiga hatua kubwa, lakini akawataka watekelezaji wa mradi huo mkoani m mwake kutobweteka badala yake kuhakikisha ujenzi unakamilika ndani ya mkataba.

Alitoa rai kwa wataalamu wanaosimamia mradi huo, kufanya kazi kwa uaminifu, weledi na kufuata sheria na kanuni, akiwaonya dhidi ya tabia ya udokozi wa fedha za miradi kwa kuwa watachukuliwa hatua.

Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Dk. Julius Ningo, aliahidi kusimamia kikamilifu mradi huo ili ukamilike kwa viwango na ubora unaolingana na fedha zilizotumika.

Ofisa Elimu Halmashauri ya Namtumbo, Juma Fulluge, aliishukuru serikali kwa kupeleka fedha nyingi za ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Mkoa wa Ruvuma.

Alisema katika awamu ya kwanza, zaidi ya Sh. bilioni 1.6 zimetolewa ambazo zimejenga vyumba 12 vya madarasa, mabweni matano, maabara tatu, vyoo na nyumba za walimu.

Alibainisha kuwa kazi inayoendelea kwa sasa ni ujenzi wa jengo la utawala na ukumbi wa shule, akitamba kuwa shule hiyo ikikamilika, itakuwa miongoni mwa shule bora mkoani Ruvuma.