Bibi harusi afa kwa ajali Arusha, vifo vyafikia 25

26Feb 2024
Na Waandishi Wetu
ARUSHA
Nipashe
Bibi harusi afa kwa ajali Arusha, vifo vyafikia 25

​​​​​​​VIFO vilivyotokana na ajali ya barabarani katika Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha vimefikia 25, huku mmoja wa waliopoteza maisha akiwa ni bibi harusi mtarajiwa, Fathiya Chucha (23).

Fathiya Chucha (23) aliyekuwa bibi harusi, akiwa ni mmoja wa waliopoteza maisha katika ajali iliyotokea Arusha mwishoni mwa wiki.

Vilevile, kati ya majeruhi waliolazwa katika Chumba cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalum (ICU) cha Hospitali ya Rufani ya Mkoa (Mount Meru), inaelezwa kuwa yumo bwana harusi, ambaye anapigania uhai wake.

Ajali hiyo iliyoacha simanzi na vilio katika Mkoa wa Arusha, ikisababisha ulemavu kwa baadhi ya majeruhi 21, ilitokea juzi saa 11:00 jioni katika eneo la Kibaoni Bypass, Ngaramtoni ya Juu, Barabara Kuu ya Namanga/Arusha.

Jana Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadhi Juma Haji, baada ya kufika katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Arusha (Mount Meru) kutoa pole kwa majeruhi, alisema vifo 10 zaidi vimeongezeka kutoka 15 vilivyoripotiwa juzi baada ya kutokea ajali.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni lori la mizigo lenye namba za usajili KAC 943 H, aina ya Mack lililokuwa linavuta tela lenye namba za usajili ZF 6778, kuyagonga magari mengine yaliyokuwa mbele yake.

Lori hilo la masafa marefu, mali ya kampuni ya KAY Construction ya Nairobi, Kenya, liligonga basi dogo la abiria (daladala) aina ya Nissan Caravan, namba T 879 DBY kisha likagonga gari dogo, aina ya Mercedes Benz (saloon) na baadaye basi la wanafunzi la Shule ya Mchepuo wa Kiingereza ya New Vission, aina ya Toyota Coaster, namba T 673 DEW lililokuwa na raia wa kigeni pamoja na watanzania.

Kwa mujibu wa Kamishna Awadhi, uchunguzi wa awali unaonesha kuwa lori hilo lilifeli breki, kitendo ambacho kilisababisha kwenda kuyagonga magari mengine.

Alisema jeshi hilo linaendelea kumsaka dereva wa lori hilo lililosababisha ajali, ambaye alikimbilia kusikojulikana muda mfupi baada ya ajali.

Kamishna Awadhi aliwataja  waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni wanaume 14, wanawake 10 na mtoto mmoja wa kike, huku raia wa kigeni waliofariki dunia wakitambuliwa ni saba.

RAIS SAMIA

Juzi Rais Samia Suluhu Hassan katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii aliandika: "Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya vifo vya watu 15 katika ajali iliyohusisha magari manne eneo la Ngaramtoni, mkoani Arusha.

"Ninatuma salamu za pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa waliopoteza jamaa zao katika ajali hii. Ajali hizi zinachukua wapendwa wetu, nguvukazi ya taifa na mihimili ya familia.

"Ninaendelea kutoa wito kwa kila mmoja kuzingatia sheria za usalama barabarani katika matumizi ya vyombo vya moto.

"Ninaagiza vyombo vyetu vya ulinzi, usalama na udhibiti kuendelea kuhakikisha vinasimamia sheria kikamilifu, ikiwamo ukaguzi wa mara kwa mara wa vyombo vya usafiri na udhibiti wa leseni kwa madereva wanaorudia kuvunja kuvunja sheria mara nyingi, na wakati mwingine kusababisha watu kupoteza maisha."

BIBI HARUSI

Katika ajali hiyo, familiya ya Latipha Mphoy, mkazi wa Kijenge Mwanama, jijini Arusha, imempoteza mtoto wao, Fathiya Chucha, aliyetarajia kufanya sherehe ya kuagwa kabla ya harusi (send off) Aprili 18, mwaka huu.

Simulizi kuhusu utambuzi wa mmoja wa waliopoteza maisha katika ajali hiyo kuwa ni bibi harusi mtarajiwa, imetokana na kundi sogezi la waliosoma Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kibosho mwaka 1995 (Kibosho Girls), kupewa taarifa ya mwanachama mwenzao kufiwa na mwanawe waliyekuwa wakimchangia fedha za kuendesha shughuli ya 'send off'.

Katika taarifa hiyo iliyochapishwa saa 2:18 usiku wa Februari 24 na Mwenyekiti wa Kundi hilo la Kibosho Girls, Asha Zulu, kulieleza kuwa ajali hiyo imeondoa maisha ya bibi harusi mtarajiwa, Fathiya Chucha; mtoto wa mwanakikundi mwenzao Latipha Mphoy, aliyekuwa kwenye gari dogo aina ya Mercedes Benz.

Kwa mujibu wa andiko hilo la kiongozi wa kundi hilo, mwili wa Fathiya ulitarajiwa kuzikwa jana saa saba mchana huko Kijenge Mwanama, jijini Arusha.

KONDAKTA ALONGA

Kondakta wa lori la mizigo lililosababisha ajali hiyo, Jastas Juma, raia wa Kenya, akisimulia hali ilivyokuwa, alisema lori lao halikuwa bovu kama inavyodaiwa.

Shuhuda huyo aliiambia Nipashe jana kuwa wakiwa njiani maeneo ya Oldonyo Sambu, moja ya magurudumu lilipata pancha na kubadilishwa na kuendelea na safari hadi walipofika Arusha Bypass, wakashtukia gari halishiki breki.

"Nikaanza kupiga kelele watu wapishe maana gari halina breki nikashtukia nimetupwa mtaroni na sikufahamu kilichoendelea na kujikuta baada ya muda nipo wodini," alisema Jastas.

Kondakta wa lori hilo alisema walikuwa wanatokea Kenya kuelekea jijini Dar es Salaam.

"Baada ya ajali mimi sikujua dereva wangu alikwenda wapi. Mimi nilijikuta tu niko kwa hospitali," alisema Jastas.

Mashuhuda wengine ambao ni majeruhi wa ajali hiyo, raia wa Togo, Apelo Apeto na Paulo Dino, raia wa Nigeria, kwa nyakati tofauti walieleza kuwa walikuwa wakitoka Shule ya New Vission iliyoko Ngaramtoni na walikuwa huko kwa ziara ya mafunzo.

"Nikiwa eneo la tukio nilisikia kishindo cha gari na sikufahamu kilichoendelea, lakini ninawashukuru madaktari na wauguzi kwani nimepata huduma nzuri na sasa ninaweza kuongea," alisema Apeto, raia wa Togo.

Alisema ziara yao ilishafikia mwisho na ilikuwa ifikapo Ijumaa wiki hii wangerejea kwenye mataifa yao.

NAIBU WAZIRI

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Juma Sagini, alimwagiza Kamishna wa Polisi wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadhi, kuhakikisha magari yote ya mizigo yanakaguliwa kwenye mipaka ya nchi inapofika ili kuepusha ajali zisizo za lazima.

Pia alitaka askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani wasisubiri wiki ya usalama barabarani kufanya ukaguzi, bali iwe desturi ya kila mara kwa magari ya ndani ya nchi.

"Lori hili lingekaguliwa Namanga pale mpakani lisingekuja kutusababishia ajali hapa kwetu limetoka huko likiwa bovu, hata kwa kuliangalia ni chakavu, lingekaguliwa haya yasingetokea, sasa ukaguzi ufanyike mipakani kwa magari haya ya mizigo," aliagiza.

* Imeandaliwa na Cynthia Mwilolozi, Godfrey Mushi (ARUSHA) na Idda Mushi (MOROGORO).