Bei sukari kubandikwa barabarani

26Feb 2024
Maulid Mmbaga
Tabora
Nipashe
Bei sukari kubandikwa barabarani

WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe, amesema taifa limeingia katika changamoto ya sukari lakini tatizo hilo ni la muda  na litakwisha.

WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe.

Amesema kuwa siku chache zijazo watatoa waraka wa kulazimisha kila mawakala na duka linalouza sukari liweke bei barabarani.

Bashe pia amesema taifa limelinda sekta ya sukari, akisisitiza wenye viwanda wanapolindwa, watambue wana wajibu kwa umma na uchumi wa taifa na si kuumiza wananchi.

Ameyasema hayo mkoani Tabora wakati wa uzinduzi wa ofisi mpya ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) iliyoanzishwa 2015 kwa lengo la kuleta mapinduzi ya kilimo kwa mipango endelevu inayokidhi mahitaji ya wakulima kupitia huduma tofauti za kifedha, kama mikopo ya moja kwa moja, yenye ushirika na dhamana.

"Kuna mtu juzi aliletewa sukari hapa halafu anaweka faida ya Sh. 5,000 kwenye mfuko, hatuwezi kuruhusi hivi, lazima tufanye ‘decentralization’ ya mifumo ya usambazaji sukari, mtu wa Kigoma anafuata sukari Kahama au Mwanza si sawa.

"Lazima waweke mawakala katika mikoa, Coca-Cola kwani tunazifuata Dar es Salaam, si tunachukua kwenye ‘depot’ hapahapa Tabora! Kwanini isiwezekane kwenye sukari? Kwanini sekta ya sukari haiguswi, imefungwa fungwa kama kitu fulani kitakatifu? Bashe amehoji.

Amesema sekta hiyo inapewa mikopo kwa wakati na kwamba benki ya TADB iliipatia mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 70 kama sehemu ya utekelezaji wa uanzishwaji wake ambao ni kutoa huduma za kifedha kwa kupitia kongani na minyororo ya thamani kwa nia ya kuleta mapinduzi ya kimkakati katika kilimo na kwa wakulima wadogo.

Waziri Bashe amesema yeye ni miongoni mwa wanaozisaidia sekta binafsi, lakini hawezi kufanya hivyo kwa zinazoumiza watu, akiwasisitiza kuwa waache kuhangaika na kama wana jambo, waende wizarani wakalijadili.

Ameeleza kuwa haiwezekani kwa baadhi ya wafanyabiashara kupewa kibali cha kuingiza sukari tani 10,000 ilhali wanaishia kuleta tani 2,000 ambazo pia zinakuja kwa mafungu.

"Ninataka niwaambie Watanzania ukweli, wanataka tupate uhaba bei iende juu, wananchi waizoee bei ya Sh. 5,000, hata hali ikirekebishika tuendelee kuinunua kwa bei hiyo, haitowezekana, hatuwezi, tuwe waungwana, lazima tutende haki.

"Na mimi niwaambie mfumo wa kibepari wowote na kuna watu wanaleta hoja wanasema 'waziri kwanini unatoa bei elekezi', pale penye ukiritimba wa bei, serikali lazima isimamie.

"Mimi niwaambie tutasaidia viwanda vyetu, tutavilinda, lakini hatutaruhusu vichukue faida ya kuumiza wananchi kutokana na changamoto iliyojitokeza.

"Nimewaambia lazima wafungue maghala, wawe na mawakala kwenye mikoa, haiwezekani mtu anasafiri zaidi ya Km 700 kwenda kufuata sukari na kurudi, hatuwezi kuruhusu aina hii ya biashara, haiwezekani!" Bashe amesisitiza.

Amesema wameshagawana maeneo hivyo wanataka kuona yanakuwa na kituo cha mauzo, mawakala zaidi ya mmoja ili wananchi wapate huduma.

"Tumewaambia wenye viwanda tunawalinda, tunataka uwazi kwenye gharama za uzalishaji, unapolindwa na kutunzwa una haki, lakini vilevile una wajibu, lazima tujue gharama zako za uzalishaji, lazima watanzania wajue tunabadili mfumo ambao haujawahi kuguswa kwa miaka 30, 40.

"Ni ngumu kupambana, lakibi tutashinda kwa uwezo wa Mungu, tumetoa nafuu ya asilimia 53, lazima hiyo nafuu tuione kwa mlaji. Rais katoa hiyo ili aipate mtanzania wa kawaida, sukari inakuja na itaendelea kuja hadi hali itakapokuwa sawa," amesema Bashe.

Benki ya TADB tangu kuanzishwa kwake, imetoa mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 284 kufadhili miradi ya kimkakati 71 na kunufaisha wakulima wadogo 1,049,370.