Mayege anadaiwa kufanya kitendo hicho kwa kile kinachodaiwa ni kutokana na mtoto huyo kulia wakati wa usiku.
Baba huyo, anadaiwa kumpiga sehemu mbalimbali za mwili mtoto huyo kwa kutumia mkanda wa suruali na kiatu na kisha kumrusha kwenye kochi, hali iliyosababisha jeraha kichwani na kumsababishia kifo.
Mzazi huyo anadaiwa kufikia hatua hiyo baada ya kukasirishwa na kitendo cha mtoto huyo kulia nyakati za usiku alipombembeleza bila kukoma, hivyo kumshushia kipigo pamoja na mama wa mtoto huyo.
Akisimulia tukio hilo, mama mzazi wa mtoto, Riziki Leonard, alisema baba huyo alifika majira ya 5:00 usiku akampakulia chakula na baada ya kula, alikwenda kulala na kukuta mtoto analia, hivyo kuanza kumbembeleza huku akimpiga makofi.
“Baada ya mtoto kuendelea kulia, alianza kumpiga makofi ya nguvu kisha kumrusha kwenye kochi ambapo tuliona amelegea lakini alimfuata pale na kuanza kumpiga kwa kiatu na mkanda akisema nitakuua, nitakuua, nikamzuia lakini hakusikia,” alisema.
Riziki aliongeza kuwa baada ya mtoto kutulia na kulegea kwenye kochi, alikwenda kumzuia lakini baba huyo hakusikia akaendelea kumpiga mikanda pamoja na mama yake ambaye pia ilimng’ata shavu la mama huyo.
Baada ya kutekeleza unyama huo, alisema mwanamume huyo alitokomea kusikojulikana hivyo kumlazimu kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa kitongoji.
Akithibitisha tukio hilo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kilimahewa, Michael Chuma, alisema alipokea taarifa kutoka kwa mwenyekiti wa kitongoji majira ya saa 7:00 usiku, hivyo kufika katika eneo la tukio na kukuta mtoto huyo akiwa tayari amefariki dunia.
Chuma alisema baada ya kubaini hivyo alitoa taarifa polisi waliofika na kuchukua mwili huo kuupeleka hospitalini kwa ajili ya vipimo zaidi huku hatua za kumtafuta mtuhumiwa zikiendelea.
“Tulibaini kuwa tayari mtuhumiwa amekimbilia kusikojulikana, hivyo Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria,” alisema Chuma.
Ndugu wa Marehemu, Emannuel Sospeter, alisema baada ya kufika hospitalini mwili ulifanyiwa uchunguzi na kubainika kuwa mtoto huyo alipata maumivu makali katika maeneo ya kichwa na jeraha la ndani hali liyosababisha damu kuvuja kwa ndani na kumsababishia kifo.









