Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Jane Byemelwa baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka yoyote.
Hakimu Byemelwa alisema mahakama hiyo inatoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo ili iwe fundisho kwake na watu wengine wenye tabia kama hizo.
Alisema Upande wa Mashtaka, ukiongozwa na Inspekta wa Polisi Zakayo Napegwa, ulipeleka mahakamani huko mashahidi watano na vielelezo vitatu ambavyo vilithibitisha kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo.
Hakimu Byemelwa alisema kuwa siku ya tukio hilo, Novemba 18, 2023, saa saba usiku, katika Kijiji cha Bunazi, Wilaya ya Missenyi, mkoani Kagera, mshtakiwa aliingia kwenye chumba cha mdogo wake (wa tumbo moja) ambaye ni msichana mwenye umri wa miaka 17 na kumkuta amelala, alimshika kwa nguvu na kumvua nguo kisha kumnajisi.
Alisema kuwa baada ya mshtakiwa huyo kunajisi mdogo wake, binti huyo alipiga kelele ndipo wazazi wao pamoja na majirani walifika eneo la tukio hilo na kukamata mshtakiwa huyo na kumpeleke Kituo cha Polisi Kyaka na alipohojiwa alikiri kuhusika na kosa hilo.
Hakimu alisema mwathirika wa tukio hilo alipewa Fomu Namba Tatu ya Polisi (PF3) na kupelekwa Kituo cha Afya Bunazi, alikofanyiwa uchunguzi na daktari na kuthibitishwa kuwa kweli alinajisiwa.
Alisema kuwa baada ya upelelezi wa kesi hiyo kukamilika, mshtakiwa alifikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Hakimu Byemelwa alisema amesikiza ushahidi wa pande zote na kubaini kuwa Upande wa Mashtaka umethibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka yoyote, hivyo mahakama inamtia hatiani mshtakiwa.
Mwendesha Mashtaka Inspekta wa Polisi, Zakayo Napengwa alidai mahakamani huko kutokuwa na kumbukumbu za makosa ya nyuma ya mshtakiwa.
Alidai kitendo alichokifanya mshtakiwa ni cha kikatili na kinadhalilisha jamii, hivyo akaomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa huyo ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine wenye tabia kama yake.
Mshtakiwa huyo wakati wa kuomba kupunguziwa adhabu, alidai ni kosa lake la kwanza, hivyo akaomba mahakama impunguzie adhabu kwa sababu ana familia inayomtegemea.
Hakimu Byemelwa alisema kitendo alichokifanya mshtakiwa hakikubaliki, ni cha aibu katika jamii, hivyo mahakama inakuhukumu kutumikia kifungo cha miaka 30 gerezani ili iwe ni fundisho kwake na kwa watu wengine wenye tabia kama zake.
Awali akisoma hati ya mashtaka, Inspekta wa Polisi Zakayo Napegwa alidai kuwa Novemba 18, 2023, saa saba mchana, kijijini Bunazi, wilayani Missenyi, mshtakiwa alinajisi mdogo wake ambaye ni msichana mwenye umri wa miaka 17 na kumsababishia maumivu makali sehemu zake za siri. Kitendo hicho ni kinyume cha sheria.